WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk Pindi Chana amewahimiza wawekezaji wa mazao ya misitu kutoka nchini China kuanzisha viwanda kwa lengo la kuuza bidhaa zilizokamilika kwa ajili ya masoko ya nje ya nchi.
Dk Chana amezungumza hayo leo Oktoba 27, wakati wa uzinduzi wa Umoja wa Wawekezaji wa Mazao ya Misitu wa China nchini Tanzania uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mji wa Mafinga mkoani Iringa.
“Nawapongeza mnaozalisha bidhaa zilizokamilika ambao tayari mna viwanda lakini tuendelee kuwekeza kwa kufuata taratibu na sheria” amesema Dk Chana huku akisisitiza “Tunataka Tanzania ya Viwanda”.
Amefafanua kuwa kupitia umoja huo mashirikiano na mahusiano kati ya Serikali na wenye viwanda yatakuwa rahisi zaidi na kusisitiza kuwa bidhaa zitakazozalishwa ziwe na nembo ya “made in Tanzania”.
Naye, Rais wa Umoja wa Wawekezaji wa Mazao ya Misitu wa China nchini Tanzania, Zheng Rongnan amesema kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania umoja huo utaboresha mazingira ya kibiashara ili kila mwananchama anufaike.
“Lengo la kuwa na umoja huu ni kuboresha, mshikamano kupanua uwekezaji, kukuza maeneo tuliyowekeza na kukuza mawasiliano baina yetu na Serikali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba amesema kuwa uwepo wa umoja huo umesaidia kukuza uchumi, kutoa ajira kwa vijana pamoja na kuongeza mchango wa Wilaya ya Mufindi katika pato la taifa.
Comments are closed.