Dk Kiruswa: Nendeni mkajifungue hospitali

NAIBU Waziri wa Madini Dk Steven Kiruswa amewataka viongozi wa mila maarufu kwa jina la Laigwanani na viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya kitongoji, kijiji na kata kuwahimiza wajawazito wa jamii ya kifugaji ya kimasai kuhakikisha wanajifungua katika vituo vya afya ili kuepusha vifo vilisivyo vya lazima.

Dk Kiruswa ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Longido alisema hayo alipokuwa katika kituo cha afya cha Ngarenaibor wilayani Longido wakati akikabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 3.5 ambavyo vinakwenda kuboresha utoaji wa huduma za afya ndani ya jimbo hilo.

Alisema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inajitahidi kutafuta mamilioni ya fedha nje kwa ajili ya wananchi wote ili kupata tiba ya uhakika na akina mama wajawazito kupata vifaa tiba vya kujifungulia lakini inasikitisha kuona baadhi ya akina mama wa jamii ya Kimasai wakijifungulia.

Naibu Waziri huyo alisema hilo haliwezekana na kuwaagiza viongozi wa mila na serikali wa ngazi zote kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii hiyo kuacha kujifungulia nyumbani na kwenda katika vituo vya afya ili kupata huduma safi na salama.

SOMA: Dk Kiruswa atoa maelekezo 5 sekta ya madini

“Hivi vifaa mvitunze na muhakikishe vinadumu na vinakwenda kutoa huduma kwa wananchi, ila muendelee kuwasisitiza wananchi wa jamii yetu ya Kimasai kuja kupata huduma ya kujifungulia katika vituo hivi vilivyojengwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuendelea kuhakikisha wanapata uzazi salama na kuepuka vifo visivyo vya lazima,” alisema Dk Kiruswa.

Sambamba na hilo Dk Kiruswa alisema ataendelea kuhakikisha anatatua mapungufu yote yaliyopo katika sekta ya afya katika jimbo la Longido likiwemo la upungufu wa watumishi ili kuweza kuziba mapungufu yote yaliyomo katika vituo vyote vya afya katika jimbo hilo lenye wakazi wengi wa jamii ya kifugaji.

SOMA: Dk Kiruswa kufunga Jukwaa la Madini               

Kwa upande wake diwani wa viti maalum jimbo la Longido, Mensiana Bendera ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwapigania wanawake kwani vifaa tiba hivyo vitakwenda kuwasaidia wanawake wa jamii ya kimasai.

Alisema jukumu walilonalo ni kuhakikisha akina mama wa jamii ya kimasai inakwenda kujifungulia katika vituo vya afya ila ombi kwa serikali ni kwa watumishi kupata nyumba za uhakika ili waweze kuifanya kazi hiyo kwa umakini kuliko hivi sasa wanatoka mbali na kushindwa kuwajibika ipasavyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido,Nassoro Shemzigwa amemuhakikishia mbunge wa jimbo hilo kuwa majengo yote ambayo hayajakamilika pamoja na mapungufu madogo yaliyoko katika vituo vya afya katika wilaya hiyo watakwenda kushirikiana na wananchi wa kata zote 18 sambamba na Baraza la Madiwani ili kuhakikisha kila kituo cha afya kinakwenda kufanya kazi kama ambavyo ilikusudiwa na serikali.

Alisema changamoto za kukosekana kwa nyumba za watumishi wa afya katika Wilaya ya Longido changamoto hiyo nayo itatafutiwa dawa ili kila mtumnishi aishi katika nyumba ya serikali ili aweze kutimiza majukumu yake ipasavyo.  

Habari Zifananazo

Back to top button