Dk Mdede arudi tena jimbo la Kalenga

IRINGA; DAKTARI kijana mwenye historia ya kuaminiwa katika uongozi na siasa, Dk Musa Leonard Mdede amechukua rasmi fomu ya kuwania uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea ubunge wa Jimbo la Kalenga katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu katika ofisi za CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Dk Mdede aliishukuru CCM kwa kuendelea kutoa nafasi kwa vijana kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi, akisema hatua hiyo inaonesha dira njema ya chama hicho katika kujenga kizazi kinachowajibika kwa taifa.

“CCM ni chama kinachoamini katika nguvu za vijana. Kupitia nafasi hii, nitaleta dira mpya, chachu ya maendeleo na msukumo wa kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na viongozi waliotangulia,” alisema Dk Mdede.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio makubwa yanayoonekana katika sekta mbalimbali nchini, ikiwemo afya, elimu na miundombinu, akisema kuwa yameongeza matumaini mapya kwa Watanzania.

Hata hivyo, alisema atasubiri ridhaa ya chama kabla ya kueleza kwa kina dira, mikakati na vipaumbele vyake katika kulijenga Jimbo la Kalenga endapo atapata nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM.

Safari ya Uongozi Dk Mdede (37), mkazi wa Kata ya Nzihi, ni daktari wa binadamu aliyebobea, akiwa mhitimu wa Shahada ya Udaktari wa Binadamu (MD) kutoka Chuo Kikuu cha CUHAS-Bugando.

Katika siasa, Dk Mdede aligombea Ubunge wa Kalenga mwaka 2015 kupitia CHADEMA na kushika nafasi ya pili, kabla ya kurejea CCM mwaka 2020 ambapo alishika nafasi ya nne kati ya wagombea 67 waliojitokeza kuomba kuteuliwa kugombea jimbo hilo.

Kwa sasa, Dk Mdede ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Iringa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, pamoja na Kamati ya Elimu na Propaganda ya UVCCM Mkoa wa Mbeya — nafasi zinazoonesha ushawishi wake katika siasa na uongozi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button