RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema ana matumaini kuwa mabadiliko ya Sheria ya Makadhi yataondoa utata na migongano ya kiutendaji katika mhimili wa Mahakama.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Charles Hilary jana ilieleza kuwa Dk Mwinyi alisema hayo Ikulu Zanzibar alipozungumza na Kamati ya Sheria mpya ya Makadhi na kupokea taarifa ya mwelekeo wa rasimu hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Wakili Mwandamizi wa Serikali, Saleh Mbaraka.
Hilary alieleza kuwa kutokana na dhamira njema iliyopo, Dk Mwinyi ana imani kuwa sheria ijayo itakuwa nzuri, yenye tija, isiyo na mivutano na yenye mwelekeo wa kujenga.
Alisema rasimu hiyo itakapofikishwa katika ngazi ya Baraza la Mapinduzi, wajumbe wa Baraza hilo watapata fursa ya kuipitia, sambamba na Kamati ya sheria ya Baraza hilo kushauri juu ya vipengele vinavyofaa kuingizwa au kupunguzwa.
Dk Mwinyi aliwashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa dhamira ya kuja na sheria mpya ya Makadhi kutokana na mahitaji yaliyopo na akasema hatua ya kuwashirikisha wadau itawezesha kupata mchango wa maoni ya kutosha
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla alisema kuongoza mhimili wa Mahakama ambamo ndani yake kuna Kadhi Mkuu kunahitajika busara.