RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inajivunia ushirikiano uliopo baina yake na India.
Dk Mwinyi alisema hayo Ikulu Zanzibar alipozungumza na Balozi mdogo wa India visiwani Zanzibar, Dk Kumar Praveen aliyefika kujitambulisha.
Alisema Zanzibar imekua ikinufaika na fursa kutoka India ikiwemo za masomo ya muda mrefu na mfupi na miradi ya maji.
Dk Mwinyi alisema sekta ya maji safi na salama ni muhimu katika ustawi wa jamii na maendeleo ya ukuaji wa uchumi Zanzibar.
Aliishukuru Serikali ya India kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa SMZ hasa ufadhili wa miradi ya maji inayotekelezwa kupitia mkopo wa Benki ya Exim ya India.
Akizungumzia ujenzi wa Taasisi ya Teknolojia ya India (India Institute Technology-IIT), inayotarajiwa kujengwa Zanzibar kwa ushirikiano wa Serikali ya India, Dk Mwinyi alimueleza Balozi Praveen kwamba mazungumzo baina ya SMZ na wahadhiri kutoka Taasisi ya Teknolojia ya India (IIT) yanaendelea vizuri.
Dk Praveen aligusia miradi ya maji Zanzibar inayofadhiliwa na Serikali ya India ukiwamo mradi wa Chuo cha Ufundi wa Amali, Pemba na ufadhili wa masomo kwa watumishi wa Zanzibar nchini India.
Balozi Praveen alimweleza Dk Mwinyi kuhusu ujio wa Waziri wa Mambo ya Nje ya India, Dk Subrahmanyam Jaishankar anayetarajiwa kuwasili nchini mwezi ujao kwa uzinduzi wa miradi ya maji Zanzibar.
Dk Subrahmanyam pia anatarajiwa kufika Dar es Salaam na Dodoma.
Uhusiano wa diplomasia baina ya Tanzania na India ni wa historia ambapo India ilifungua Ubalozi wake Dar es Salaam Novemba mwaka 1962 na mwaka 1974 ikafungua ubalozi mdogo Zanzibar.
Ushirikiano huo umeendelea kuimarika kwa fursa nyingi za maendeleo kupatikana kwa watu wa mataifa hayo mawili.
Tanzania inaongoza kwa kupata nafasi nyingi za udhamini wa masomo nchini India kuliko nchi nyingine yoyote barani Afrika.