Dk Mwinyi asifu uzalendo wa Charles Hilary

MAMIA ya waombolezaji wamemzika aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Charles Hilary (65) kwenye makaburi ya Mwanakwerekwe Mkoa wa Mjini Magharibi.

Charles aliaga dunia Mei 11, mwaka huu wakati akipata matibabu katika Hospitali ya Muhimbili Mloganzila mkoani Dar es Salaam.

Kabla ya maziko, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alisema anajuta kutomweleza, Charles kuwa alikuwa mtu mzuri.

Dk Mwinyi alisema hayo wakati wa ibada ya kuaga mwili wa Charles katika Viwanja vya Mapinduzi Square mjini Unguja jana.

“Kuna fundisho tunalipata hasa kwenye misiba, fundisho lenyewe ni kwamba tuwe tayari kuwasifu na kuwaambia wafanyakazi wetu wakifanya vizuri palepale, tusingoje mpaka mtu katangulia mbele ya haki ndiyo tunatoa sifa zake,” alisema Dk Mwinyi.

Aliongeza: “Nasema kama kuna jambo nalijutia ni kutomwambia Charles mapema… tumeondokewa na mtu mzuri, mcheshi mchapakazi na hodari wa kazi yake, lakini ndiyo mapenzi ya Mungu”.

Alisema, Charles alikuwa mtu mzuri na mchapakazi na amemsifu kwa uzalendo wake.

“Nilimpigia simu mwenyewe nikamwambia nakuhitaji uje kunisaidia… hakusita alijibu palepale, na mimi nilimwambia kidiplomasia kidogo nikamwambia tafakari kisha uje kunijibu, akanambia kwa ‘heshima uliyonipa nakujibu sasa hivi kwamba niko tayari kuja kufanya kazi na wewe’, namshukuru sana marehemu kwa moyo wake wa kizalendo kuja kuitumikia nchi yake,” alisema Dk Mwinyi.

Amemshukuru mmiliki wa Kampuni ya Azam Media, Abubakar Bakhresa kwa kumruhusu Charles afanye kazi Ikulu licha ya kuwa bado walimhitaji.

“Hakusita kunambia (Bakhresa) maadam unamuhitaji sisi pia tunamuhitaji, lakini tunakupa maana kazi unayompa ni ya nchi tuko tayari kumuachia. Nakushukuru, Abubakar kuniruhusu kumtumia Charles miaka minne,” alisema Dk Mwinyi.

Ameahidi kumuenzi, Charles kwa kutimiza aliyomuomba aifanyie familia yake.

“Kwenye familia sikupata nafasi ya kukutana na mkewe wala mtoto, lakini nilikuwa nawajua sababu alikuwa akiwazungumzia sana, alinipa ombi linalohusiana na familia yake… nitakuja kuzungumza na ninyi (familia), nimelipokea lakini nataka niwahakikishie kwamba nitamuenzi kwa kazi aliyonifanyia kwa kutimiza yale aliyoyataka juu ya familia yake,” alieleza Dk Mwinyi.

Alisema, Charles alikuwa mfanyakazi mzuri na wote wanatambua kazi aliyofanya kwenye uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Tukiwa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM watu wote walifurahia kazi nzuri na sauti nzuri iliyowekwa na Charles, tutamkumbuka alikuwa mtu anajituma na mara zote akihakikisha majukumu yake yanafanyika vizuri,” alisema Dk Mwinyi.

Aliongeza: “Pamoja na majukumu na kazi nzito na kwa ofisi yangu yenye mambo mengi ‘stress’ ni kawaida, lakini mbele ya marehemu Charles tulikuwa tunacheka, tunafurahi”.

Charles Hilary aliyezaliwa Oktoba 22, 1959 Jang’ombe mjini Unguja kwa baba mwenyeji wa Morogoro na mama mwenyeji wa Zanzibar, alikuwa mtangazaji maarufu nchini aliyefanya kazi Radio Tanzania (RTD), Radio One, Deutsche Welle (DW), BBC na Azam kabla ya kuteuliwa na Rais Mwinyi kwenda Ikulu mwaka 2021.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button