Dk Mwinyi ataka jamii isaidie wasiojiweza

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema jukumu la kuwasaidia watu na makundi yenye uhitaji ni la jamii nzima na kuwataka wenye uwezo kufanya hivyo ili kupata fadhila za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Dk Mwinyi alisema hayo jana wakati akizungumza na makundi maalumu yenye uhitaji yakiwamo ya wazee, wajane, watoto yatima na wenye ulemavu katika Viwanja vya Mapinduzi Square katika Mkoa wa Mjini Magharibi baada ya kuwakabidhi msaada wa vyakula uliotolewa na Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa ya Zanzibar.

Alisema kwa kuwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni wa neema, inampendeza Mwenyezi Mungu kuishi kwa upendo, ushirikiano na kusaidiana hususani kusaidia jamii za watu wenye uhitaji kwa kila mtu na uwezo aliojaliwa na Mwenyezi Mungu.

Advertisement

Mmoja wa wanufaika wa msaada huo, Jamila Boraafya alimshukuru Rais Mwinyi kwa jitihada anazozifanya ili kuwafikia wananchi na makundi yote katika jamii na kueleza kuwa kiongozi huyo amekuwa mfano wa kuigwa.