Dk Norga Komba: Mji wa serikali Dodoma, nguzo ya Tanzania ya kisasa

DODOMA: Kwa zaidi ya miongo mitano, Dodoma imebeba ndoto kubwa ya kuwa kitovu cha utawala na maendeleo ya Tanzania. Ndoto hiyo, iliyoasisiwa mwaka 1973 na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, leo inashuhudia sura mpya ya mafanikio.
Dodoma ya sasa siyo tu makao makuu ya Serikali, bali ni ishara ya dira ya taifa, uthubutu wa uongozi na dhamira ya Tanzania ya kujenga nchi ya kisasa inayokwenda sambamba na mahitaji ya karne ya 21. Ukuaji wa mji huo unaendelea kufungua milango ya uwekezaji, biashara, teknolojia na ushirikiano wa kimataifa, huku ukiimarisha nafasi yake kama moyo wa shughuli kitaifa.
Hayo ni sehemu ya mtazamo wa Dk Norga Komba, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) China, anayeeleza kuwa uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba Oktoba 30, 2026, uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ni alama muhimu katika safari hiyo ya kihistoria.

RAIS Dk Samia Suluhu Hassan akikata utepe pamoja na mgeni wake, João Manuel Conçalves Lourenço, Rais wa Jamhuri ya Angola kuashiria ufunguzi wa Majengo ya Ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma jana.
Kwa mtazamo wake, hatua hiyo ni ushahidi wa namna maono ya muda mrefu yanavyoweza kutafsiriwa kuwa matokeo halisi na urithi wa maendeleo kwa Watanzania wa kizazi cha sasa na vijavyo.
MJI WA SERIKALI MTUMBA NA SURA MPYA YA UTAWALA
Anasema kuwa uamuzi wa kuifanya Dodoma makao makuu ya Tanzania ulitangazwa ukiwa ni sehemu ya maono makubwa ya kujenga mji mkuu unaowakilisha umoja, maendeleo na mustakabali wa taifa.
Hatua ya kuhamishia shughuli za Serikali Dodoma, iliyoimarishwa mwaka 2016 na kukamilisha hatua kubwa za uhamishaji mwaka 2019, ilifungua ukurasa mpya katika historia ya utawala wa Tanzania.
Katika kuendeleza azma hiyo, Serikali ilianza mwaka 2021 ujenzi wa awamu ya pili ya majengo ya kisasa ya wizara na taasisi mbalimbali katika Mji wa Serikali Mtumba. Uwekezaji huo mkubwa umejenga mazingira mapya ya utendaji wa Serikali na kuziweka taasisi muhimu karibu zaidi katika kitovu kimoja cha utawala.
Kwa mujibu wa taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, uwekezaji katika mradi huo umefikia takribani Sh bilioni 700, ukiwa na takribani kilomita 59 za barabara pamoja na mifumo ya kisasa ya mawasiliano.

Aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi barabara kati ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa niaba ya Serikali na China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) ya China, kwa lengo la kutekeleza upanuzi wa barabara ya njia sita jijini Dodoma Mei 2026.
Dk Norga Komba anaona mafanikio hayo kuwa hatua muhimu katika kuimarisha mazingira ya utendaji wa taasisi za umma na kuwezesha shughuli za Serikali kuratibiwa katika eneo moja.
Kwa maana hiyo, Mji wa Serikali Mtumba ni zaidi ya mkusanyiko wa majengo ya kisasa. Ni ishara ya Tanzania inayojenga taasisi imara, inayowekeza katika ufanisi wa utawala na kuweka msingi wa maendeleo endelevu.
TEKNOLOJIA NA TASWIRA YA SERIKALI YA KISASA
Katika dunia inayobadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia, Tanzania inaendelea kuwekeza katika mifumo ya kisasa inayorahisisha utendaji wa Serikali.
Mji wa Serikali Mtumba umejengwa katika mazingira yanayozingatia mifumo ya kisasa ya mawasiliano na teknolojia, hatua inayofungua ukurasa mpya katika safari ya Serikali ya kidijitali.
Muunganiko wa wizara na taasisi mbalimbali katika eneo moja una uwezo wa kuimarisha mawasiliano, kurahisisha uratibu wa shughuli na kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Muonekano wa Majengo ya Ofisi za Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na Barabara katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.
Katika eneo hili, Dk Norga Komba anaeleza kuwa teknolojia inakuwa daraja muhimu linalounganisha taasisi, watumishi na wananchi. Kadiri mifumo ya kidijitali inavyoendelea kuimarika, ndivyo Tanzania inavyojenga Serikali inayokwenda sambamba na kasi ya dunia ya kisasa.
“Hii ndiyo taswira ya Dodoma mpya: mji mkuu unaojengwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa, huku ukiweka msingi imara kwa mahitaji ya kesho,” anasema Dk Norga Komba.
DODOMA NA FURSA MPYA ZA UCHUMI NA UWEKEZAJI
Anaeleza ukuaji wa Dodoma kama makao makuu ya nchi unaendelea kuleta sura mpya katika uchumi wa jiji na maeneo yanayolizunguka.
Kadiri shughuli za Serikali, taasisi, wageni na wawekezaji zinavyozidi kuongezeka, ndivyo mahitaji ya makazi, hoteli, usafiri, huduma za kifedha, teknolojia na biashara mbalimbali yanavyoendelea kukua.
Dk Norga Komba anasema hiyo ni fursa muhimu kwa sekta binafsi, wajasiriamali na wananchi kushiriki katika uchumi unaopanuka. Biashara ndogo na za kati, kampuni za ujenzi, watoa huduma za teknolojia na wawekezaji katika sekta mbalimbali wanaendelea kupata nafasi katika ukuaji wa jiji hilo.

Sehemu ya muonekano wa jiji la Dodoma, huku shughuli za kiuchumi zikiendelea. Hii ni uthibitisho kuwa Dodoma imendelea kukuwa kila iitwapo leo.
Kwa Dk Norga Komba, ukuaji huo unajenga mnyororo mpana wa fursa unaogusa sekta mbalimbali za uchumi. Anaeleza kuwa mji mkuu unazidi kuwa kitovu cha uwekezaji, ubunifu na biashara, huku ukichochea ajira na kuongeza shughuli za kiuchumi.
MIUNDOMBINU NA MUUNGANIKO WA KITAIFA
Anafafanua kuwa taswira ya Tanzania ya kisasa inaonekana pia katika uwekezaji mkubwa wa miundombinu unaoendelea kuunganisha Dodoma na maeneo mbalimbali ya nchi.
Reli ya Kisasa (SGR), Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, barabara za kisasa na miundombinu ya mijini vinaendelea kuimarisha nafasi ya Dodoma kama kitovu cha muunganiko wa kitaifa.

Muonekano wa Uwanja wa Ndege Msalato ambao hadi Septemba 2026 ulifikia asilimia 89.02 za ujenzi wake.
Hatua hiyo imepata sura ya kipekee zaidi kupitia uzinduzi wa barabara za Mji wa Serikali Mtumba, uliofanywa tarehe 30 Oktoba 2026 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Angola, João Lourenço.
Barabara hizo, zilizojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), zina urefu wa kilomita 59.1. Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, miundombinu hiyo inajumuisha kilomita 11.7 za barabara za njia mbili na kilomita 36 za barabara za njia moja.
Zaidi ya kuunganisha majengo na taasisi za Serikali, barabara hizo zimejengwa kwa mtazamo mpana wa huduma za kisasa na mazingira rafiki kwa wananchi. Mradi huo umejumuisha vituo 52 vya mabasi, taa 1,635 za barabarani, kilomita 59.1 za njia za watembea kwa miguu pamoja na kilomita 59.1 za njia za waendesha baiskeli.

Picha ikionesha Mji wa Serikali Mtumba, pamoja na miundombinu ya barabara zenye ubora zinazozunguka mji huo.
Aidha, katika kuimarisha ustahimilivu wa miundombinu dhidi ya athari za mazingira, mabwawa matatu ya kuzuia mafuriko yamejengwa katika eneo la Mji wa Serikali. Hii inaonesha namna mipango ya maendeleo ya mji inavyoweza kuunganisha mahitaji ya usafiri, usalama wa wananchi na maandalizi dhidi ya changamoto za mazingira.
Uamuzi wa kuzipa baadhi ya barabara hizo majina ya viongozi wakuu wa kitaifa waliotoa mchango mkubwa katika historia ya Tanzania, akiwemo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, unaongeza thamani ya kihistoria katika maendeleo hayo. Ni muunganiko wa kumbukumbu ya safari ya taifa na taswira ya Tanzania inayojengwa kwa ajili ya siku zijazo.
Miundombinu hiyo inaifanya Dodoma kuwa rahisi kufikika na kuunganisha mji huo na vituo vya uzalishaji, masoko na maeneo mengine ya Tanzania.
Pia, mipango ya kuboresha usafiri wa mijini inaonesha dhamira ya kuhakikisha ukuaji wa jiji unaendana na mahitaji ya wananchi. Uwekezaji katika usafiri, miundombinu ya watembea kwa miguu na muunganiko wa maeneo mbalimbali unajenga mazingira bora zaidi ya maisha na shughuli za kiuchumi na huu ni utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Kwa mtazamo wa Dk Norga Komba, haya ni maendeleo yanayothibitisha kuwa Dodoma haijengwi kwa ajili ya leo pekee, bali kwa ajili ya Tanzania ya vizazi vijavyo.
DODOMA KATIKA RAMANI YA DIPLOMASIA NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Kama makao makuu ya Serikali, Dodoma inaendelea kujijenga kama jukwaa muhimu la diplomasia, ushirikiano wa kimataifa na majadiliano ya ngazi za juu.
Miji mikuu duniani ni vituo vya maamuzi, mikutano ya kimataifa na ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi. Dodoma nayo inaendelea kujenga mazingira yanayoiwezesha Tanzania kupokea wageni wa kimataifa, ujumbe wa kidiplomasia, wawekezaji na taasisi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Uwepo wa Mji wa Serikali Mtumba na miundombinu mingine ya kisasa unaimarisha taswira ya Tanzania kama taifa linaloendelea kujenga mazingira bora ya utawala na ushirikiano wa kimataifa.

Muonekano wa majengo ya Mji wa Serikali Mtumba baada ya uzinduzi wake jana Oktoba 30, uliofanywa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
Dk Norga Komba anabainisha kuwa ushiriki wa Rais wa Angola, João Lourenço, katika uzinduzi wa Mji wa Serikali Mtumba na barabara zake tarehe 30 Oktoba 2026, ni mfano wa namna Dodoma inavyozidi kuimarisha nafasi yake katika shughuli za kidiplomasia na ushirikiano wa kimataifa.
DODOMA: URITHI WA MAONO NA MUSTAKABALI WA TAIFA
Mji wa Serikali Mtumba ni sehemu ya safari ndefu ya Tanzania katika kutimiza maono ya kujenga makao makuu ya kisasa, yenye uwezo wa kubeba mahitaji ya taifa linalokua.
Leo, Dodoma inasimama kama ushahidi kwamba maono makubwa yanahitaji uamuzi, uongozi na uwekezaji wa muda mrefu ili kuwa halisi.
Zaidi ya kuwa makao makuu ya Serikali, Dodoma ni ishara ya Tanzania inayobadilika. Ni kitovu cha utawala, fursa za kiuchumi, teknolojia, miundombinu na ushirikiano wa kimataifa.
Kadiri majengo ya kisasa yanavyoendelea kusimama, barabara na reli zinavyoimarika, na shughuli za kiuchumi zinavyozidi kukua, ndivyo taswira ya Dodoma mpya inavyozidi kujidhihirisha.
Katika kuhitimisha mtazamo wake, Dk Norga Komba anaeleza kuwa Mji wa Serikali Dodoma ni zaidi ya mradi wa miundombinu. Ni nguzo ya Tanzania ya kisasa, ishara ya maono yaliyotimia na urithi wa maendeleo unaoendelea kujengwa kwa ajili ya Watanzania wa leo na vizazi vya kesho.



