SPIKA wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson ameiomba serikali kupitia Rais, Dk Samia Suluhu Hassan kuboresha barabara chakavu za mitaa ya Jimbo hilo ambazo ni zaidi ya km 400.
Dk Tulia amesema hayo wakati wa kilele cha maonesho na sherehe za wakulima Nanenane kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya jana Agosti 8, 2023.
Pamoja na ombi hilo, Dk Tulia amemshukuru Rais Samia na serikali yake ya kwa kufanikisha uboreshwaji wa sekta mbalimbali katika jiji hilo ikiwemo elimu, afya na zaidi kutoa Sh trilioni 1.1 kwa ajili ya kujenga barabara ya njia nne kutokea Igawa hadi Tunduma yenye urefu wa KM 218.
Kuhusu uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Dk Tulia amemueleza Rais Samia kwamba Wananchi wa Mbeya wamemuagiza amueleze kwamba wameukubali na kuubariki uwekezaji huo wenye maslahi mapana kwa taifa.
Akijibu ombi hilo, Rais Samia ameahidi kwenda kujipanga na serikali yake ili kuona namna ambayo wataweza kufanya maboresho hayo ya barabara za mitaa ya Jiji hilo.