Dola milioni 8 kukuza biashara
DAR ES SALAAM: SERIKALI ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), imesema itatoa uwekezaji wa Dola milioni 8.3 kwa kampuni kadhaa Tanzania ili kukuza biashara.
Fedha hizo pia zitasaidia kuboresha usalama wa chakula, na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika nyanja ya mauzo ya nje kupitia Mpango wa Kufikia masoko ya Marekani (Agoa).
Mkurugenzi wa Misheni ya USAID Tanzania Craig Hart amesema hayo leo Dar es Salaam na kuongeza kuwa kampuni tisa za ndani zitapata ruzuku chini ya Mradi wa Biashara na Uwekezaji wa USAID Afrika.
SOMA: USAID yaipiga ‘jeki’ shule ya wasichana Sega
Alizitaja baadhi ya kampuni hizo kuwa ni BioBuu, Biotan Limited, Central Park Beew, Minjingu Mines na Fertilizer Limited, Mount Meru Millers, na Red Earth Limited.
“Tunasherehekea ushirikiano wa USAID na makampuni tisa katika sekta muhimu, ikiwa ni pamoja na asali, korosho na nguo, ambayo yanatarajiwa kuzalisha ajira 2000, na kukuza hadhi ya Tanzania kama kitovu cha uchumi wa kanda,” amesema.
Amesema kupitia fursa ya Soko la Agoa, wanasaidia kampuni ya Kitanzania kutafuta masoko Amerika.
“Agoa ni sehemu muhimu ya sera ya kiuchumi ya Marekani na Afrika, inayozipa nchi zinazostahiki zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara usafirishaji wa bidhaa bila ushuru katika soko la Marekani kwa bidhaa zaidi ya 1800,” amesema.
#DYK @USAID provides assistance to address the food security and nutrition needs of refugees in Tanzania’s Nduta and Nyarugusu camps, including children ages five years and younger, pregnant and lactating women, and other vulnerable groups. #USwithTanzania #WorldHumanitarianDay pic.twitter.com/Pq8PYgdAms
— USAIDTanzania (@USAIDTanzania) August 19, 2024
Wakati huo huo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo, amesema mafanikio kupitia Mradi wa Biashara na Uwekezaji wa USAID Afrika (ATI) bado kuna kazi kubwa ya kufanywa ili kutumia kikamilifu uwezekano wa biashara na uwekezaji nchini.
“Kuna haja ya kuendelea kukuza na kuimarisha uwezo wetu wa uzalishaji na ugavi ili kukidhi mahitaji ya soko, kubadilisha kiwango Cha mauzo ya nje kwa kupanua zaidi na kujumuisha bidhaa zilizoongezwa thamani na viwango vya juu, ili kuimarisha ustahimilivu wa ugavi” amesema.
Amesema kuna haja ya kuimarisha miundombinu kwa kuwekeza katika usafirishaji, vifaa, na uunganishaji wa kidijitali ili kurahisisha biashara na kupunguza gharama, na kukuza uvumbuzi na ujasiriamali kwa kuhimiza maendeleo ya bidhaa na huduma mpya ili kukidhi mahitaji yanayoendelea ya soko la Marekani na kwingineko.