Dorothy Semu: Wanawake tuwe huru kugombea
DAR ES SALAAM: “Tunatakiwa kuwa huru kugombea nafasi yoyote ndani chama, wanaume wanapaswa kuamini kwa kushirikiana na wanawake wataleta mabadiliko na maendeleo chanya katika jamii yetu,” amesema Kiongozi wa Chama Cha ACT- Wazalendo, Dorothy Semu.
Akiwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mjadala mfupi kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na Taasisi ya TGNP ambayo yaliyoanza Agosti 14, 2024 kiongozi huyo amesema mfumo wa ACT- Wazalendo katika nafasi za uongozi umewawezesha wanawake pia upo kuwawezesha wenye uwezo zaidi ili kuongoza kwa ufanisi zaidi.
“Sera yetu ya jinsia imeona namna gani fursa wanawake waliopo kwenye vyama vya siasa na ambao hawapo kwenye majukwaa ya kisiasa ili tushirikiane kwa pamoja. Kupitia nafasi ninayoongoza ni lazima nifanye mazingira kuwa wezeshi ili yeyote atakayekuja katika jukwaa la kiongozi akute mazingira bora asipitie changamoto ambazo nimepitia au walizopitia wengine,”amesema Semu.
SOMA: ACT Wazalendo yavuna CCM, CUF Mchinga
Dorothy Semu amesema kuna haja ya kushirikiana, katika kazi ili kuliletea taifa maendeleo. Amesema anaamini mwanamke ana nafasi kubwa katika kuongoza na anaweza kuongoza.
Mafunzo hayo yanayolenga kuwajengea uwezo viongozi juu ya umuhimu wa ushiriki wa wanawake kwenye uongozi na ngazi za maamuzi ya serikali za mtaa yatadumu kwa siku tatu.