WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama, ameitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuwa kioo na kitovu cha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) nchini.
Jenista alitoa kauli hiyo jijini Dodoma mara baada ya Mkurugenzi Mkuu wa e-GA, Benedict Ndomba kuwasilisha mada kuhusu usalama wa serikali mtandao kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, iliyolenga kuwajengea uwezo viongozi hao kuhusu usalama wa mitandao.
“Tunataka e-GA iongeze ubunifu na ujengaji wa mifumo ya Tehama ili kuwa kitovu cha utafiti kwa ukanda wa Afrika Mashariki, pamoja na kazi kubwa na nzuri ambayo e-GA inaifanya lakini inapaswa kuongeza juhudi zaidi,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Daniel Sillo alisema ameridhishwa na utendaji kazi wa e-GA na kuitaka kuendelea kuwa wabunifu na kuhakikisha usalama wa mifumo ya Tehama ili kudhibiti upotevu wa fedha za serikali hasa katika halmashauri.
Akiwasilisha mada kuhusu usalama wa serikali mtandao, Ndomba alisema hivi sasa kuna ongezeko la vitendo vya udukuzi wa taarifa mbalimbali ambapo amewasihi wabunge na wananchi kwa jumla kuwa makini na matumizi ya Tehama pamoja na taarifa wanazopata mitandaoni.
Aidha, wajumbe wa kamati hiyo waliipongeza e-GA kwa kutekeleza vema majukumu yake na kuitaka kutoa elimu kuhusu usalama wa mitandao kwa wananchi ili kuwajengea uelewa na kuweza kulinda taarifa zao katika mitandao.