Ester Thomas: Juhudi zinahitajika kulinda demokrasia

NAIBU Katibu Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Bara, Ester Thomas ametoa wito wa kuimarisha juhudi za kulinda demokrasia nchini.

Sambamba na hilo amepongeza juhudi zilizofanyika tangu enzi za waasisi wa taifa kwa kupigania demokrasia, ikiwamo kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

Esther ametoa wito huo leo wakati akizungumza katika mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania ambao umewakutanisha wadau mbalimbali katika Ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kujadili hali ya demokrasia nchini kwa mwaka mmoja uliopita.

SOMA: ACT- Wazalendo wateua manaibu katibu wakuu Bara, Zanzibar

“Sote tumesikia neno hili demokrasia toka zamani likitamkwa hata kabla ya uanzishwaji wa vyama vya siasa mwaka 1992. Tuwaenzi waasisi na viongozi mbalimbali waliopigania demokrasia, wengine walitangulia mbele za haki na wengine bado wako hai,” amesema Esther.

Akizungumza kuhusu mafanikio ya hivi karibuni, ameelezea kuwa kumekuwa na maendeleo mazuri katika kupigania demokrasia, ikiwamo maboresho ya sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa.

Aidha, ametambua mchango wa vyombo vya habari katika kueneza demokrasia, akisema kwamba vyombo hivyo vinasaidia kwa kiasi kikubwa kuipa sauti demokrasia nchini.

Hata hivyo, Esther amezungumzia changamoto zinazoikabili demokrasia nchini, akitaja vikwazo vya vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara bila kuingiliwa na vyombo vya dola. Amesisitiza kuwa vitisho na matukio ya utekwaji yanaibua hofu na kuathiri demokrasia.

“Licha ya mafanikio haya, kumekuwa na mvutano katika maeneo kadhaa. Kwanza, vikwazo dhidi ya vyama vya siasa, hasa upinzani, kufanya mikutano ya hadhara bila kusumbuliwa na vyombo vya dola'” ameeleza Ester.

Habari Zifananazo

Back to top button