Feisal achangisha fedha aishitaki Yanga

KIUNGO wa Yanga mwenye mgogoro na klabu hiyo,  Feisal Salum maarufu Feitoto, amewaomba mashabiki wake na mashabiki wa mpira wa miguu nchini kumchangia fedha zitakazomuwezesha kwenda kufungua kesi katika Mahakama ya Usuluhishi Michezoni (CAS),ili kuvunja mkataba wake na Yanga.

Amesema amefikia hatua hiyo kwa vile Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), limeshindwa kumsaidia hivyo ameamua kwenda CAS na kudai haki yake na kuomba wadau wamsaidie.

Kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagramu ameandika: “Ndugu zangu Watanzania na familia yote ya soka kwa Bara na visiwani. Mimi kijana wenu ambaye kwa miaka yote nimekua na nidhamu nje na ndani ya uwanja na kwa dhati nimeitumikia klabu ya Yanga na Timu ya Taifa ya Tanzania na Zanzibar Heroes.

“Utiifu wangu umekua shubiri ya maisha yangu ya soka, nimevumilia nimeshindwa, sitamani tena mama yangu kutukanwa. TFF imeshindwa kunisaidia kupata haki yangu ya Kuvunja mkataba na Yanga hivyo nimeamua Kwenda Mahakama ya michezo CAS.

“Nahitaji Mchango wa kila Mtanzania mpenda haki na maendeleo ya wachezaji wa Kitanzania ambao wamekua kimya na woga juu ya maslahi, Heshima na Haki zao.

Naomba unichangie kadiri utakavyoweza ili niweze kupata pesa ya Kulipia gharama za kufungua Jalada la kesi yangu CAS ili kupata Haki yangu ya Kuondoka Yanga kwa kuvunja mkataba.

“Tafadhali naomba unichangie ili nipate haki yangu itakayoniwezesha kutumikia kipaji changu na Timu za Taifa (Tanzania na Zanzibar) katika namna tofauti kwa manufaa yangu na Taifa. Shangazi Fatma Karume na wanasheria wengine watafanya kazi Bure.

Unaweza kulipia kwa lipa namba (5406394 FEISAL SALUM) hapo pichani au kwa namba hii ya simu kwa Tigo Pesa 067 912 8899 FEISAL SALUM ABDALLAH,” ameandika nyota huyo..
.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button