Fid Q, Lord Eyes waja na ‘Neno’

Wanamuziki wa muziki wa Hip Hop Tanzania, Fid Q na Lord Eyes usiku wa Novemba 02 2024 kwa pamoja wametambulisha vionjo kadhaa vilivyomo kwenye album yao ya kwanza iitwayo ‘Neno’  ambayo inatarajiwa kutoka hivi karibuni.

Vionjo hivyo ni baadhi ya vitu vinavyopatikana kwenye album yao ya Neno yenye nyimbo 15 na vionjo vilivyotolewa leo ni nyimbo 7 tu kwa ajili ya Wadau wachache walioalikwa kuja kusikiliza wakiwemo viongozi wa serikali, mabalozi mbalimbali, wasanii na waandishi wa habari.

Advertisement

Akizungumza na waandishi wa habari, Rappa Fid Q amesema ‘leo tumewaonjesha wadau nyimbo 7 kutoka kwenye album yetu yenye nyimbo 15 na baada ya hapa, mashabiki wa muziki wategemee kuona tour ya Fid Q na Lord Eyes tukiwafata hukohuko waliko’ – Fid Q

Upande wa Lord Eyes amesema: ‘Huu ni mradi mkubwa, ndani ya albamu hii kuna albamu 3 ndani yake, itakuja na Filamu fupi, nia yetu kufanya mapinduzi ya muziki wa hip hop Tanzania, Neno the Album inakuja hivi karibuni.”

Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma akiwasilisha salaam za Rais Samia amesema  ‘Rais anafurahia kuona Watanzania wanafurahi kupitia sanaa ya nchi yao na sisi kama wizara tutahakikisha hivi vitu havikwami sehemu yoyote na tutaunga mkono kwa asilimia mia’,” Mwana FA.

Nyimbo zilizotambulishwa leo usiku wa Neno Experience ni pamoja na Glory RMX, Cheupe, Okey na dunia na baadhi ya wasanii walioshirikishwa kwenye album hiyo ni pamoja na Damian Soul, Zahir Ally Zoro na Melissa John.