MAREKANI : FILAMU ya “No Other Land,” inayoangazia mateso ya Wapalestina kutoka kwa wanajeshi wa Israel, imeibuka mshindi wa tuzo ya Oscar.
Filamu hii, iliyotayarishwa kwa miaka mitano, inaonyesha jinsi wanajeshi wa Israel wanavyobomoa nyumba za Wapalestina na kuwafurusha ili kuunda maeneo ya mafunzo ya kijeshi na kutoa nafasi kwa walowezi wa Kiyahudi.
Mmoja wa waongozaji wa filamu hiyo, Basel Adra kutoka Palestina, alisema: “Filamu hii inaonyesha ukweli mgumu ambao tumekuwa tukivumilia kwa miongo mingi. Tunatoa wito kwa dunia kuchukua hatua kukomesha dhuluma hii kwa Wapalestina.”
Mwenzake, Yuval Abraham kutoka Israel, aliongeza: “Tulifanya kazi hii kwa pamoja, Wapalestina na Waisraeli, kwa sababu sauti zetu kwa pamoja zina nguvu zaidi. Tunaona uharibifu wa Gaza, na lazima hii ikomeshwe.”
Alisema pia: “Tunaishi katika mazingira tofauti – mimi niko huru chini ya sheria za kiraia, lakini Basel anateseka chini ya sheria za kijeshi.”
Naye Waziri wa Utamaduni wa Israel, Miki Zohar, alikosoa filamu hiyo na kusema ni “mtazamo potofu kuhusu Israel.” SOMA: Israel, Hamas mambo safi
Ingawa filamu hiyo imeshinda tuzo kubwa, haijapata wasambazaji nchini Marekani. Abraham alisema hii inatokana na sababu za kisiasa, lakini ana matumaini hali hiyo itabadilika.