Gamondi: Tabora ni ndogo ila tunawaheshimu

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema licha ya kwamba wanawazidi Tabora United kwa ubora wataingia uwanjani katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Novemba 7 kwa kuwaheshimu kuhakikisha wanapata pointi tatu.

Gamondi amesema hayo leo Dar es Salaam kuelekea mchezo huo kwenye Uwanja wa Azam Complex.

“Yanga ndio timu kubwa Tanzania, tunafahamu Tabora ni timu ndogo lakini lazima tuwaheshimu, najua wanaweza kuja na kuzuia zaidi ili tusiwafunge kisha watushambulie kwa kutushtukiza. Tumejiandaa kwa namna yoyote ile watakayokuja nayo, lengo ni pointi tatu.”amesema.

Advertisement

SOMA: Pazia Ligi Kuu bara kufunguliwa leo

Amesema Yanga imefanya kadiri ya uwezo wake kurejea kwenye ubora na imeshafanya tathmini ya kutosha kubaini ubora wa wapinzani, kilichobaki ni kufanyia kazi kutimiza lengo la kusalia kileleni mwa ligi.

Gamondi amesema Tabora wamebadilika kimbinu kwani wametoka kushinda mechi mbili za mwisho wakiwa nyumbani. Msimu huu wamefunga magoli tisa lakini wameruhusu magoli 14.

“Nafikiri kocha wao mpya anacheza kwa tahadhari zaidi. Tumejiandaa vyema na ni matumaini yangu tutapata alama tatu muhimu,”amesema.

Kocha wa magolikipa wa Tabora United, Khalifan Mbonde amesema wamekuja kupambana, wamejiandaa vizuri ili kupata matokeo.

“Kusudi letu ni tofauti, tumejiandaa japo tumetoka kwenye mchezo mgumu hivi karibuni ila tuko tayari na tunawaheshimu Yanga sana hivyo tumekuja kupambana,”amesema.