CHAMA cha Ushirika cha Geita (GCU) kimeadhimia kuwekeza katika kilimo cha alizeti kama zao mbadala la kuongeza kipato cha ushirika na wakulima kuondokana na utegemezi wa kilimo cha pamba pekee.
Meneja wa GCU, Venance Musiba ameeleza hayo mara baada ya mkutano mkuu wa mwaka kwa wanachama wa GCU waliokutana mjini Geita kujadili mwelekeo na maendeleo ya chama.
Musiba amesema wanachama wameridhia mpango huo na kupitisha maadhimio ya GCU kuomba mkopo wa Sh milioni 530 kwa ajili ya kununua mitambo ya kukamua mafuta kutoka mbegu za alizeti.
Amesema mitambo hiyo ya kukamua mafuta ya alizeti itawekwa katika eneo lililokuwa la kiwanda cha pamba cha ushirika Geita ili kurejesha uhai wa kiwanda sambamba na kutoa ajira kwa vijana.
“Lengo kubwa tulilonalo tunataka kuanza kuzalisha mbegu za alizeti, mwakani tumepanga kulima hekari 200 za alizeti, kwa kuanza nazo, na tumeshawasiliana na watafiti wa mbegu waweze kutuzalishia mbegu.
“Alizeti ni zao jingine la kimkakati, na ni zao ambalo linakusudiwa kuwaongeza kipato wakulima wetu, kwani wakulima wakiwa na mazao mengi, hata tegemeo la kipato kwa wakulima linakuwa kubwa.”
Ameeleza wakati wa msimu wa mavuno GCU itanunua alizeti kutoka kwa wakulima na kuzisindika ili kuziongeza thamani, na kisha kukamua kupata mafuta ambayo ndiyo itakuwa bidhaa kikuu ya ushirika.
Mkaguzi kutoka Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) kanda ya ziwa, Reuben Kemincha alisema taarifa ya ukaguzi ya machi 2022 ilibaini mapato yote ya GCU ni sh milioni 257 kwa mwaka.
Amesema wamebaini matumizi ni sh milioni 393 na hasara ni sh milioni 136 inayotokana na uchakavu wa mali mbalimbali za ushirika ikiwemo kiwanda cha ushirika ambacho kikifufuliwa kitaondoa hasara.
Mkulima wa Chama Cha Msingi Bukoli, Marco Shimo amekiri kuridhishwa na malengo ya kufufua na kubadili kilichiokuwa kiwanda cha pamba Kasamwa ili kianze kukamua mafuta ya alizeti.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Josephat Katwale ame GCU kuweka mbele mipango yenye maslahi kwa wakulima ili kupanua uwigo wa uzalishaji na masoko kwenye sekta hiyo.