Goli moja tuu litatupeleka robo fainali-Ahmed
DAR ES SALAAM: Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba Ahmed Ally amesema wamejiandaa kikamilifu kumnyoa Jwaneng Galaxy siku ya Jumamosi katika Uwanja wa Benjamini Mkapa ili kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akiwa katika tukio la uzinduzi wa wiki ya hamasa kuelekea mchezo huo jijini Dar es Salaam Ahmed amesema kinachohitajika kwa timu hiyo ni kuvuna ushindi wa aina yoyote ili kuipata tiketi ya robo fainali kisha mengine yatafuata.
“Wydad kuruhusu magoli mawili tulipomfunga, shughuli yake iliishia pale, hata atume mwakilishi kwenye mechi ya Jwaneng hakuna kitakachobadilika. Hatuna presha ya kufunga magoli mengi, goli moja tu linatosha.” Amesema Ahmed na kuongeza
“Goli moja tu litatupeleka robo baada ya hapo tunatafuta magoli ya kufurahi, goli la pili, goli la tatu.
Hata hivyo Simba wanaingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kuondoshwa katika michuano hiyo na Jwaneng Galaxy licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 nchini Botswana walijikuta wakitandikwa 3-1 na kushidwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2021.