Gwajima asisitiza ushiriki wanawake sekta ya majini

DAR ES SALAAM: Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, amehimiza kuimarishwa kwa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi, akitaka wapewe fursa zaidi za kushika nafasi za kitaalamu, usimamizi na uongozi katika sekta mbalimbali, ikiwemo usafiri wa majini.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Jumuiya ya Wanawake Wanaofanya Kazi katika Sekta ya Usafiri wa Majini Kusini na Mashariki mwa Afrika (WOMESA), Gwajima amesema Tanzania imepiga hatua katika kuongeza uwakilishi wa wanawake kwenye uongozi.
Amesema wanawake wanashikilia takribani asilimia 40 ya nafasi za ubunge nchini, akieleza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kuendelezwa kwa kupanua uwakilishi wao katika bodi za taasisi na maeneo mengine ya kufanya maamuzi.

Amesisitiza pia umuhimu wa kuhakikisha wanawake wanapata nafasi sawa za kugombea na kuchaguliwa katika uchaguzi wa viongozi wa jumuiya hiyo, akieleza kuwa uwakilishi wao utaimarisha sauti ya wanawake katika mijadala na maamuzi yanayohusu maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini.
Kwa upande wake, Rais wa WOMESA, Dk. Deother Edward, amesema mkutano huo unalenga kufanya Mkutano Mkuu wa Mwaka pamoja na kukusanya na kuchakata takwimu zinazohusu ajira katika sekta ya usafiri wa majini.
Amesema mkutano huo umewakutanisha washiriki kutoka nchi 17 za Kusini na Mashariki mwa Afrika, hatua inayotoa fursa ya kujadili hali ya ajira na nafasi za wanawake katika sekta hiyo.



