Gwajima: Pato la taifa linateketea kupambana na ukatili

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima amesema serikali za nchi zimekuwa zikitumia asilimia 3.5 ya pato la taifa kwa ajili ya kupambana na ukatili wa kijinsia.

Gwajima ameyasema hayo leo Novemba 25, 2023 jijini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa Kampeni ya siku 16 za Kupinga ukatili wa Kijinsia, ambapo amesema kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia asilimia 2 ya pato linakwenda kwenye mapambano ya kijinsia huku nchi zikitumia asilimia 3.5

Advertisement

“Mnataka ajira, mnataka miundombinu mizuri, mnataka elimu bora, mnataka huduma za afya, maji na huduma nyingine muhimu lakini nyie wenyewe mnashindwa kujizuia mioyo yenu kufanya ukatili, unakuta mtu anabaka, mtu anampiga mpaka kumpa ulemavu mwenzake, mmeshajiuliza ni gharama kiasi gani serikali yetu inapoteza kwa ajili ya kupambana na ukatili?” amesema kwa kuhoji na kuongeza

“Tanzania haitasaonga mbele kama vitendo vya ukatili wa kijinsia havitatokomezwa, wote kwa pamoja tunapaswa kushikamana kutokomeza vitendo hivi, mila, desturi kandamizi ndio zinatupa umaskini,”amesema

Aidha, amesema ukatili bado ni janga kubwa nchini na kwamba takwimu za utafiti wa Hali ya Idadi ya Watu na Afya, 2022 inaonyesha asilimia 27 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wamekumbwa na vitendo vya ukatili wa kimwili kuanzia walipokuwa na umri wa miaka 15.

Hata hivyo amesema takwimu hizo zimepungua kutoka asilimia 40 mwaka 2015 hadi asilimia 27 mwaka 2022.

Amesema, wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 asilimia 12 wamewahi kukumbana na vitendo vya ukatili wa kingono, wakati kwa upande wa majumbani asilimia 39 ya wanawake wameripotiwa kukumbana na vitendo vya ukatili kutoka kwa wenza wao wa sasa ama waliopita.

“Ripoti inaonyesha vitendo vya ukeketaji ni asilimia nane, mimba za utotoni zimepungua kutoka asilimia 27 hadi asilimia 22, tatizo bado lipo, kama serikali bado tunapambana, uwepo wa vitendo hivi vya ukatili vinachangiwa na mfumo dume na unyonge wa kiuchumi,”amesema.

Amesema serikali kwa kuona hilo mwaka 2022 imetoa mkopo wa Sh bilioni 14 kwa vikundi vya ujasiriamali vya wanawake na walemavu, ili kuwainua kiuchumi.

Kwa upande wa Mratibu wa Kitaifa wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) Anna Kulaya amesema takwimu zinaonyesha asilimia 48 ya wanawake na asilimia 32 ya wanaume bado wanaamini kuwa mwanamke akitoka bila kuaga au kuunguza chakula anapaswa kuadhibiwa.

Nae, Balozi wa Switzerland Tanzania Didier Chassot, amesema katika kila nchi, hatua zaidi zinahitajika ili kuhakikisha watu wote wanaishi bila ukatili.

2 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *