‘Hakuna upendeleo maalum kwa walimu wa kujitolea’

SERIKALI imesema kuwa ajira 13,390 za walimu zilizotangazwa hivi karibuni zitaenda kwa waliokidhi vigezo na sifa stahiki kwa walioomba na hakutakuwepo upendeleo maalum kwa wanaojitolea.

Akijibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mbunge wa Babati Vijijini, Daniel Sillo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Deogratius Ndejembi amesema kuwa endapo wanaojitolea na wameomba nafasi hizo na wanakidhi vigezo watapata ajira ila si kwa upendeleo maalum.

Katika maswali yake ya nyongeza, Sillo alitaka kufahamu ikiwa serikali itatoa upendeleo maalum kwa walimu wanaojitolea jimboni mwake na mpango wa serikali kuongeza idadi ya walimu wa kike ambao baadhi ya shule zina mwalimu mmoja tu wa jinsia hiyo.

Akijibu hayo, Ndejembi amesema: “Wanaojitolea kama wameomba ajira hizi na wanakidhi vigezo vilivyopo katika tangazo la ajira basi nao watapata. Hakutakuwemo upendeleo maalum kwa wale tu wanaojitolea ili kuweka usawa kwa wote,” ameeleza.

Amesema wilaya ya Babati ilifanikiwa kupata walimu 50 na kwamba katika nafasi zilizotangazwa hivi karibuni zitapunguza kero hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button