Halmashauri 112 hazina maambukizi, matende mabusha

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imesitisha kampeni ya umezeshaji wa kingatiba za ugonjwa wa mabusha na matende katika Halmashauri ya Jiji la Da es Salaam katika Manispaa ya Temeke na kata 10 za Manispaa ya Kinondoni ambazo hazina maambukizi mapya ya ugonjwa huo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema hayo leo Machi 12, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari juu ya hatua zilizofikiwa za kutokomeza ugonjwa wa matende na mabusha nchini hususan katika Mkoa wa Dar Es Salaam.

“Serikali kwa kushirikiana na Wadau tumeweza kudhibiti ugonjwa huu katika Halmashauri 112 kati ya 119 a kubakiwa na Halmashauri saba ambapo mafanikio hayo yamechangiwa na kampeni za utoaji elimu na umezaji kingatiba za ugonjwa huo zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi,” amesema Waziri Ummy.

Advertisement

Ummy Aidha, Waziri Ummy amesema bado kuna baadhi ya halmashauri ambazo bado zina maambukizi mapya ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na Pangani, Mafia, Kinondoni, Kilwa, Lindi Manispaa, Mtama na Mtwara Mikindani ambapo kwa ujumla kata hizo zina wakazi 1,203,359.

“Natoa rai kwa wakazi wa maeneo hayo ambayo bado kuna maambukizi ya ugonjwa huu kujitokeza kwa wingi ili kushiriki kwenye kampeni za kingatiba ya ugonjwa wa matende na mabusha zitakazoendelea kufanyika katika maeneo yao ili kuweza kutokomeza maambukizi maya va ugoniwa huu.”