Mchengerwa: Bajeti 26/27 izingatie Bima ya Afya kwa Wote

MWANZA: WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amewaagiza watumishi wa afya nchini kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 inatakiwa kuonyesha mwelekeo wa taifa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Mchengerwa amesema hayo leo Mei 3, 2026 wakati wa uzinduzi wa Kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara ya Afya jijini Mwanza.
“Katika bajeti ya 2026/2027, vipaumbele vyetu lazima vionyeshe mwelekeo wa Taifa. Kwanza, lazima tujiandae kikamilifu kwa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Hili si suala la kadi pekee; ni suala la uwezo wa mfumo. Lazima miundombinu iwe tayari,” amesema Mchengerwa.
Amesema ni lazima mifumo ya TEHAMA iwe imara pia dawa zipatikane na rasilimali watu wawepo pamoja na vifaa vya kufanyia kazi. Ameagiza mkazo katika uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya.
“Taifa lisilojenga uwezo wa kuzalisha dawa na vifaa tiba vyake, daima litakuwa mateka wa bei, usafirishaji na misukosuko ya dunia. Kwa hiyo, ununuzi kupitia MSD na mifumo yetu ya manunuzi lazima uanze kutoa msukumo wa kimkakati kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini, bila kushusha ubora,” ameongeza.
Alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026, wamefanikiwa kupiga hatua muhimu ikiwemo kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu kufikia wastani wa asilimia 73 kwa mwezi Februari, 2026.
“Tumeendelea kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kupitia uwekezaji katika vituo vya afya, hospitali za wilaya, vifaa tiba na rasilimali watu. Haya ni mafanikio ya pamoja. ” amesema.
Ametoa wito kwa kila mtumishi, kuanzia Makao Makuu hadi hospitali za rufaa, kutoka idara hadi kituo cha afya, kuhakikisha wanatoa huduma kwa weledi na huruma.
“Hatutavumilia ucheleweshaji wa huduma usio na sababu. Hatutavumilia upendeleo unaodhalilisha haki ya mwananchi.
Alisema kuna malalamiko katika sehemu mbalimbali kuhusu matumizi mabaya ya madaraka, vitisho, unyanyasaji na tabia za
kuwadhalilisha watumishi wa ngazi za chini.
Naye katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt Seif Shekalaghe amesema kikao hicho kitajadili na kupitia mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2026/2027, kikilenga kuboresha huduma za afya na ustawi wa watumishi.
Amesema watajadili kikao Tathmini ya utendaji kazi wa mwaka uliopita pamoja na kupokea mrejesho wa utekelezaji wa majukumu ya wizara. Alisema watapitisha mapendekezo ya bajeti yenye lengo la kuwanufaisha Watanzania.



