Heko Rais Samia kuokoa Watanzania Sudan

NIMEAMUA kuandika makala haya, kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuokoa maisha ya Watanzania wenzetu waliokuwa nchini Sudan, ambapo Taifa hilo limekumbwa na mgogoro mkubwa wababe wa kivita wakigombea madaraka.

Kwa hatua hii, Rais Dk Samia atabaki katika kumbukumbu sio tu kwa Watanzania wale waliokuwa Sudan, bali kwa jamii nzima kwani si katika mambo ambayo yamezoeleka, huko nyuma Watanzania waliokuwa katika nchi zenye machafuko walihangaika kunusuru maisha yao bila msaada wowote.

Ndege ya Shirika letu, ATCL, ilitua Ethiopia kuwachukua raia wenzetu na kuwarejesha nyumbani wakiwa salama. Hii ndio moja ya wajibu wa lazima wa serikali kuwalinda raia wake katika hali yoyote ile.

Tumejisikia fahari kubwa kwa kitendo hiki cha serikali, ambapo huko nyuma kila mmoja angekuwa anatafuta njia zake za manusura.

Katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa J.K. Nyerere walipokelewa na Serikali. Nilimuona Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na wasaidizi wake akiwapokea raia wenzetu hawa.

Wazazi, walezi na kila mmoja hapa alikuwa kiroho juu,  hatujui hatma ya wenzetu,tuliposikia kuwa serikali imepeleka ndege kwenda kuwachukua, kila mmoja alishukuru.

Kwa hakika, Rais Dk Samia ni kiongozi mwenye huruma, upendo, mchapakazi, mzalendo ambaye siku zote amekuwa akituonesha jinsi kiongozi wa umma anavyotakiwa awe.

Rais Dk  Samia ni mwenye utu, anajali na zaidi ni kiongozi anaesimamia hasa kulinda Katiba, sheria, mila, desturi, silka  na utamaduni wetu.

Hapo zamani niliwahi kusoma ‘ Operesheni Entebe’ pale Serikali ya Israel ilipokwenda kuwaokoa raia wake nchini Uganda wakati huo Uganda ikiwa chini ya Iddi Amin.

Tukio la kuwaokoa Watanzania hawa waliokuwa katikati ya mashaka na hatari ya maisha ni moja ya ‘operesheni’   makini iliyosimamiwa na Wizara yetu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharik

 

Nampongeza Balozi wetu wa Sudan, Silima Haji Kombo kwa kusimamia kwa weledi ‘operesheni’ ya kuwaokoa Watanzania wenzetu.

Wakati Balozi Silima akichukua jitihada hizo, wapo wenzetu wengine wanamlaumu kwanini amerejea nchini, eti angebakia Khartoum!

Nawauliza, wangekuwa wao wangebaki? Au kwa sababu wao hawapo katika uwanja wa vita?

Nchi imechafuka, kila mmoja anakimbia kunusuru maisha yake, iweje iwe kiroja kwa Balozi wetu Silima kurejea nchini?

Uamuzi wake na wa serikali ni sahihi kabisa kumrejesha nyumbani maana Khartoum kwa sasa hana kitakachomuweka  maana wenyeweji wake walompokea ni ‘ hamkani tupu’!

Nimelichomekea hili hapa kwa sababu niliona maneno maneno ya kumlaumu Balozi Silima katika baadhi ya mitandao.

Heko Rais Dk Samia kuwaokoa Watanzania wenzetu waliokuwa katika hatari nchini Sudan. Muungwana ni vitendo.

*Mwandishi amepata kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) Zanzibar.

Habari Zifananazo

Back to top button