Hersi: Aziz Ki anabaki

DAR ES SALAAM; RAIS wa Yanga, Hersi Said amesema ana matumaini makubwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Stephan Aziz Ki ataendelea kusalia kwenye kikosi cha timu hiyo msimu ujao.

Mkataba wa nyota huyo wa zamani wa Asec Mimosas ya Ivory Coast na Yanga umefikia kikomo na tayari yuko kwenye mazungumzo ya kusaini kandarasi mpya.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa Kombe la Toyota, Afrika Kusini hivi karibuni, Hersi alisema mazungumzo ya kumwongezea mkataba Aziz Ki yanaenda vizuri na ana imani atarejea nchini kwa utambulisho.

“Tuna imani kubwa ya kubaki naye, maongezi yanaendelea vizuri lakini hakuna kilichokamilika, soka ni biashara na zipo timu zenye fedha ambazo zinaweza kubadili mawazo ya Aziz Ki,” alisema Hersi.

Mbali na kuweka wazi imani ya kumbakisha nyota huyo, Hersi alifichua kuwa bado hajasaini mkataba mpya na klabu mbalimbali zikiwemo za Afrika Kusini zilizoonesha nia ya kuwania saini yake.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti kiungo huyo ameonesha kuwa ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Yanga msimu ujao.

Mara ya kwanza kwenye kile kilichoonekana kama kufichua usajili wa Prince Dube Yanga alizungumza kwenye video fupi akifurahia usajili wa nyota huyo na kuwaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa msimu ujao yeye kazi yake itakuwa kumtengenezea nafasi za kufunga mshambuliaji huyo.

Mara nyingine aliandika kwenye akaunti yake ya Instagram akimkaribisha kiungo Clatous Chama ambaye naye alimjibu anafurahia kucheza na mfungaji huyo bora wa Ligi Kuu msimu ujao.

Habari Zifananazo

Back to top button