Hitilafu ya umeme chanzo foleni vituo vya gesi

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limefafanua kuwa msongamano wa magari uliotokea hivi karibuni kwenye vituo vya kujazia gesi, ulitokana na hitilafu ya umeme katika kituo cha uwanja wa ndege kilichopo Dar es Salaam.
Akitolewa ufafanuzi wa changamoto hiyo leo Oktoba 3, jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi, Emmanuel Gilbert amesema wametoa fursa kwa kampuni zaidi ya 40 kuwekeza kwenye sekta hiyo lakini mwitikio bado umekuwa ni mdogo.

“Mwaka juzi mwishoni tulifanya maamuzi mahususi kwamba hatutaweza sisi wenyewe kama TPDC kuilisha nchi na kutoa huduma ya vituo kila tunapotakiwa kwa hiyo tukafungua milango kwa sekta binafsi ziweze kuingiza mitaji kwa sababu tunajua ni wepesi kwenye utekelezaji, mpaka sasa tumetoa idhini kwa takribani kampuni 40 lakini bahati mbaya mwitikio mdogo,”amesema Gilbert.
SOMA: Wabunge: Serikali iagize magari yanayotumia gesi
Mkurugenzi huyo ameeleza uchache wa vituo vya kujazia gesi ambapo mpaka kufikia sasa makadario ya magari ni 4,800 yanayotumia gesi ambapo uwezo wa vituo vitatu ni kuhudumia magari 1,200 hadi 1,500.



