SERIKALI kupitia Wizara ya Afya inafanya juhudi za kuhakikisha hospitali zote nchini zinakua na wodi maalum za uangalizi wa watoto njiti (NICU) na kushuka hadi katika ngazi ya jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya,Ummy Mwalimu leo jijini Dar es Salam wakati wa maandalizi ya awamu ya pili ya kuendelea kugawa vifaa tiba katika hospitali zenye wodi ya uangalizi maalum kwa watoto njiti.
“Tunataka hospitali zote nchini ziwe na huduma za uangalizi maalum kwa watoto njiti na tunashuka hadi ngazi ya msingi kama vituo vya afya kwa kuwa asilimia 70 ya wanawake wajawazito wanajifungua katika zahanati na vituo vya afya,” ameeleza Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema Rais Dk Samia Suluhu Hassan ametoa Sh Bil 6.3 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya kuanzisha wodi maalum kwa watoto njiti.
“Kwa kweli tunamshukuru Mhe. Rais Dk Samia kwa kutupa fedha hizo na tayari tumeshanunua vifaa tiba, tumeanza kuvisambaza na tunaendelea kusambaza katika hospitali zetu zaidi ya 80 nchi nzima,” amesema Waziri Ummy.
Amewataka wanawake wajawazito wote nchini kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya, kupata huduma mapema ikiwa mjamzito ana tatizo, ili wataalamu waokoe maisha ya watoto na mama.
“Tunaweza kuokoa maisha ya watoto wetu wachanga na watoto njiti endapo mjamzito atawahi kupatiwa huduma mapema, kwa wakati na huduma sahihi,” amesisitiza.