Huduma za kijamii kuwasogeza wamasai Tanga

BAADHI ya wànanchi wa jamii ya kifugaji ya Kimasai wakazi wa vijiji viwili vya Irkeepusi na Orchaniomeok vilivyoko katika kata ya Nainokanoka wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wamesema watahamia Msomera mkoani Tanga kwa hiari kwa kuwa wameridhishwa na uwepo wa huduma muhimu za kijamii.

Wamesema wameridhia wenyewe kwenda Tanga, baada ya kupata fursa ya kuwatembele wenzao waliohama ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Samweli Lazier, mkazi wa kijiji cha lrkeepusi, kata ya Nainokanoka alisema amepata fursa ya kuwatembele wenzao na ameridhishwa na mazingira ya huko.

“Nilipofika Msomera nimekuta wenzetu waliotoka huku Ngorongoro wanafanya shughuli zao mbalimbali za kujipatia kipato ikiwemo kilimo, ufugaji na biashara ndogo ndogo kwa kuwa ni sehemu ambayo mtu anakuwa na uhuru kufanya shughuli yoyote pia kuna huduma muhimu za kijamii,”

“Nimeshuhudia kuna umeme, maji, shule na miundombinu bora ya barabara hakika ni sehemu nzuri ya kuishi. “alisema Laizer

Naye Gesuma Turmeyi alisema kutokana na uzuri wa eneo ambalo wanalitakiwa kwenda kuishi, ameiomba serikali kuharakisha utaratibu wa waliojiandikisha ili waondoke.

“Hapa Ngorongoro huwezi kuwa na hatimiliki ya ardhi kukata miti au kulima hivyo nimekubali kuondoka ili nikapate fursa ya kulima na kumiliki aridhi na kufanya mambo yangu mengine,”alisema.

Metuo Setayi mkazi wa kijiji cha Orchaniomelok, kata ya Alalilai alisema anataka kuondoka ndani ya eneo la NCAA kwa kuwa amekumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kupoteza mifugo yake iliyouawa na wanyama wakali wa porini.

“Nataka kuondoka haraka iwezekanavyo kama itawezekana kwa kuwa ngo’mbe wangu watatu waliuawa na mbogo na ndama mmoja alikufa kwa kukosa majani na nimebaki maskini sina kitu kabisa,”alisema Setayi.

Alisema faida ya kwenda kuishi kwenye makazi hayo yaliyotengwa na serikali ataishi kwa furaha na amani akiwa na familia yake.

Habari Zifananazo

Back to top button