ICJ yaunga mkono Guinea ya Ikweta

UHOLANZI : MAHAKAMA ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imeamua kuunga mkono upande wa Guinea ya Ikweta katika mzozo wa muda mrefu na Jamhuri ya Gabon kuhusu umiliki wa visiwa vya Mbanie, Cocotiers na Conga.
Mataifa hayo mawili ya Afrika Magharibi yamekuwa yakizozania visiwa hivyo tangu miaka ya 1970. Ingawa visiwa hivyo ni vidogo, havikaliki, na vina ukubwa mdogo ikiwemo kisiwa cha Mbanie chenye hekta 30 ambavyo vipo katika ukanda unaosemekana kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta na gesi asilia.
Chanzo cha mzozo huo kilianzia mwaka 1900, kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa mipaka mjini Paris baina ya wakoloni wa wakati huo, Ufaransa na Uhispania. Hata hivyo, Gabon baadaye ilidai kuwa Mkataba wa Bata wa mwaka 1974 ulithibitisha kuwa visiwa hivyo ni sehemu ya ardhi yake.
Katika uamuzi wake, Mahakama ya ICJ imeeleza kuwa Mkataba wa Bata haukuwa mkataba rasmi wa kisheria unaoweza kuthibitisha umiliki wa visiwa hivyo, bali ni makubaliano yasiyo na nguvu ya kisheria.
Kwa mujibu wa mahakama hiyo, hati halali ya umiliki wa visiwa hivyo ilikuwa mikononi mwa Uhispania, ambayo baada ya kuipa Guinea ya Ikweta uhuru mwaka 1968, ilipitisha umiliki huo kwa taifa hilo jipya.
Tofauti na kesi nyingi zinazowasilishwa mbele ya ICJ ambapo hukumu hutolewa baada ya mvutano mkubwa, Guinea ya Ikweta na Gabon zilikubaliana kwa pamoja kuiomba mahakama hiyo kutoa uamuzi ili kusaidia kumaliza mzozo huo kwa njia ya amani.
Uamuzi huu wa mahakama unatarajiwa kusaidia kuondoa mvutano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo jirani na kuweka msingi wa ushirikiano wa amani katika ukanda huo wa Afrika Magharibi.
SOMA: Tanzania, Guinea Ikweta kuimarisha diplomasia