Ilani ziwe mwongozo wa kampeni uchaguzi mkuu

MEI 30, mwaka huu wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa wamepitisha na kuzindua rasmi ilani ya utekelezaji ya chama hicho ya mwaka 2025-2030 katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Akizungumza kabla ya kusoma ilani hiyo, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo anasema ilani hiyo ya saba kama zilivyokuwa nyingine za nyuma inaongozwa na dira ya kuiona Tanzania yenye ustawi kwa wote, inayozingatia na kuheshimu utu, haki na usawa na taifa imara linalojitegemea na kuheshimika kimataifa.

Profesa Kitila anasema kama ilivyo kwa vyama vingine vya siasa, CCM ilishiriki kikamilifu katika mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 hivyo ilani hiyo ni nyenzo ya kuanza utekelezaji wa dira na kuongeza kuwa sehemu kubwa na maudhui yake imetokana na maoni ya wananchama wa CCM, wananchi na wadau mbalimbali.

Anasema mbali na kushirikisha wadau ilani hiyo ni matokeo ya utafiti ambao ulilenga kukusanya maoni ya wananchi kisayansi, kuhusu masuala na maeneo ambayo wangetaka yazingatiwe katika ilani mpya ya uchaguzi. “Kwa kifupi niseme kwamba pamoja na kwamba imeandaliwa na CCM ilani hii imeakisi matamanio na matarajio ya wananchi, ni ilani ya Watanzania,” anasema.

Profesa Kitila anasema maudhui ya ilani hiyo yamezingaia kikamilifu mwelekeo wa sera za CCM ya mwaka 2020-
2030 ambayo inasimamia kujenga uchumi wa kitaifa ambao ni fungamanishi, jumuishi wenye kuleta mapinduzi katika viwanda na huduma.

Anasema ilani hiyo pamoja na mambo mengine imebeba ajenda tofauti ikiwemo kuchochea uchumi wa kisasa ulio fungamanishi na jumuishi, kuongeza fursa za ajira kwa vijana, kuongeza kipato kwa wananchi na kupunguza umasikini. Pia, kuna ajenda ya kuboresha maisha ya watu na ustawi wa jamii miundombinu ya Usafiri na Usafirishaji.

Katika mafanikio ya ilani iliyopita Profesa kitila anasema ilani ya CCM imewezesha serikali kukuza uchumi kutoka asilimia 4.8 mwaka 2020 hadi 5.4 mwaka 2024, na hivyo kuhimili athari za janga la Covid 19 na majanga mengine yaliyoikumba dunia.

Aidha, anasema pia serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi, hali iliyoongeza idadi miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutoka miradi 207 yenye thamani ya Dola za Marekani takribani bilioni 1.09 mwaka 2020 hadi miradi 901 yenye thamani ya Dola za Marekani takribani bilioni 9.31 mwaka 2024,inayotarajiwa kuzalisha ajira 212,293.

Sambamba na hayo, utoshelevu na usalama wa chakula nchini kutoka umeongezeka kutoka asilimia 114 mwaka 2020 hadi asilimia 128 mwaka 2024 hali iliyochangiwa na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani 18,665,217 mwaka 2020 hadi tani 22,804,316.

Profesa Kitila anasema hayo yametokana na juhudi za serikali katika uwezeshaji kwenye kilimo ikiwa ni pamoja na kuongeza matumizi ya mbolea, kuongeza eneo la kilimo, kuongeza upatikanaji wa mbegu bora na kuongeza bei za mazao mbalimbali.

Pia, kupitia ilani ya CCM iliyopita serikali imefanikiwa kuongezeka mauzo ya nyama nje ya nchi kutoka tani 1,774 mwaka 2021 hadi tani 14,701 mwaka 2024 sambamba na ongezeko la uzalishaji wa umeme kutoka megawati 1,602.32 mwaka 2020 hadi megawati 3,077.96 mwaka 2024 kutokana na kukamilika kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwamo mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzali sha megawati 2,115.

Yapo mafanikio katika maeneo mengi yaliyoanishwa kwenye ilani iliyopita lakini kwa upande wa kuwezesha wananchi kuongeza kipato na kupunguza umasikini serikali iliendelea kutoa ruzuku kwa kaya masikini kupitia Mpango Maalumu wa Kunusuru kaya Masikini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Profesa Kitila anasema katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2024 Sh zaidi ya Sh bilioni 9.6 zilitolewa kwa kaya masikini kupitia mpango huo na kunufaisha wananchi 5,202,655 sambamba na kutoa mikopo ya isiyo na riba kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu ambapo kiasi cha Sh bilioni 240.9 zilitolewa.

Kwa upande wa ajira, serikali ilitengeneza ajira 8,084,203 katika sekta rasmi na isiyo rasmi. Ni wazi kwamba ilani iliyopita imekuwa dira yenye mchango mkubwa kwa serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kutoa huduma bora kwa wananchi katika kipindi cha miaka mitano.

Kuzinduliwa kwa ilani mpya ambayo inapaswa kuwa dira ya utekelezaji wa serikali kwa miaka mitano ijayo, ni mwanzo wa mbio mpya za CCM kuomba nafasi nyingine ya kushika hatamu kupitia wagombea wake; Rais Samia Suluhu Hassan kwa upande wa Bara na Dk Hussein Mwinyi kwa upande wa Visiwani.

Hakuna ubishi kwamba sasa ndiyo wakati mwafaka wa vyama vyote vinavyowania nafasi katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Mwaka 2025, kufanya maandalizi na kutangaza ilani zao watakazozitumia wakati wa kampeni.

CCM wameshaianika ilani yao na wananchi wanasubiri kwa hamu ilani za vyama vingine ili kujua yaliyomo ili ziwaongoze kufanya uamuzi sahihi katika sanduku la kura itakapofika Oktoba mwaka huu. Bila shaka ilani hizo ndiyo zitakuwa mwongozo kwa wagombea wa vyama vyote kujenga hoja katika kunadi sera zao na kuwashawishi wananchi kuwaweka madarakani kulingana na yale yaliyomo kwenye ilani zao.

Ilani hizo zinapaswa kuwa dira zitakazojenga heshima kwenye majukwaa ya kampeni na kupunguza siasa za majitaka zenye kusababisha udhalilishaji na kutezwa utu miongoni mwa wagombea na viongozi wa vyama.

Ni vyema vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki uchaguzi mkuu vihakikishe vinajenga hoja thabiti kupitia ilani zao katika kuomba kura badala ya kutumia hoja za matusi au zenye kuchafuana. CCM imeshapiga kipenga cha ilani, wapigakura wanasubiri ilani za vyama vingine ziwekwe mezani ili kutofautisha maji na mafuta na mwisho wa siku wajue ni nani wanakwenda naye.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button