Inawezekana, unywaji kiasi pombe kuepuka ajali

DAR ES SALAAM: KWA mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) ajali za barabarani zinakisiwa kusababisha vifo vya watu 32.9 kwa kila watu 100,000 Tanzania.

Hali hiyo imeisukuma Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kusisitiza unywaji kiasi wa pombe kwa kuanzisha programu ya ‘Unywaji wa Pombe Kistaarabu’ iliyozalisha kampeni ya ‘Inawezekana’.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mahusiano wa SBL, John Wanyancha amesema kampeni hiyo inalenga kuwafikia vijana na wateja wengine.

“Lengo ni kuwaelezea hatari za kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa na kuwahamasisha kuchukua hatua za usalama wanapotumia vyombo hivyo… SBL kama mdau muhimu, pia hatuko mbali katika jitihada hizi ndiyo maana tumekuja na kampeni hii kuongeza usalama wa Watanzania na mali zao,” amesema Wanyancha.

Amefafanua kuwa SBL pamoja na kuwa kampuni ya kutengeneza na kuuza bia, inatambua wajibu wa kuhamasisha wateja wake kunywa kwa kiasi ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo nchini.

Kampeni hii tayari imeshafika katika mikoa ya Arusha, Moshi (Kilimanjaro) na Dodoma; ikihusisha uelimishaji kwa njia ya burudani, mijadala na wadau mbalimbali kama polisi, madereva, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), wazazi, walimu, wanafunzi na umma kwa ujumla.

Naye Meneja wa Mawasiliano na Uendelevu wa kampuni hiyo, Rispa Hatibu amesema, “SBL ipo mstari wa mbele kushirikiana na serikali pamoja na wadau wengine kuhakikisha jamii, hasa madereva wanaokunywa huku wakiendesha magari wanaelimishwa juu ya hatari za kuendesha wakiwa wamelewa na kusisitiziwa juu ya uendeshaji salama.”

Ameongeza kwamba, “Kampuni yetu muda wote itakuwa tayari kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali, ili kupunguza vifo, majeruhi na hasara kubwa inayosababishwa na ajali zinazoweza kuzuilika.”

Takwimu zinaonesha kuwa, asilimia 40 ya waathirika wa ajali za barabarani ni watembea kwa miguu huku asilimia 60 iliyobakia ni kwa watumiaji wengine wa barabara kama vile waendesha bodaboda, baiskeli na magari.

Takwimu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi zinaonesha mwaka 2023 pekee, zimetokea ajali 1,641 na kusababisha vifo vya watu 1,550 wakiwemo wanaume 1,189 na wanawake 361.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Madereva nchini, Abdallah Lubala amesema ajali za barabarani zinasababishwa na mambo mengi lakini sababu za msingi ni makosa ya kibinadamu ikiwemo ulevi, makosa ya kimiundombinu, vyombo husika vya usafiri, uzembe wa madereva pamoja na makosa ya wasimamizi wa sheria.

SOMA: Ajali za bodaboda bado tishio

Habari Zifananazo

Back to top button