INEC yaombwa kusimamia haki, usawa, uadilifu

DODOMA : TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeombwa kuhakikisha inatenda haki, usawa na uadilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
Hayo yalisemwa na Mchungaji Merick Zitto wa Kanisa la TAG – Eagle Mission Mbunyuni Kizota Dodoma akizungumza na waandishi wa habari kwenye ibada maalumu ya kumshukuru Mungu kwa kufikisha miaka 40 ya utumishi wake pamoja na miaka miwili toka kuanzishwa kwa kanisa hilo.
Amesema kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu ni matarajio ya walio wengi kushiriki kupiga kura kuchagua viongozi kwa maslahi ya taifa na maendeleo ya wananchi “Watanzania hawatahitaji kuona na kusikia INEC wanashindwa kusimamia sheria, haki, usawa kwa vyama vyote vitakavyoshiriki uchaguzi mkuu,” alisema.
Aliongeza: “Pamoja na kuwa na vyombo mbalimbali vya kisheria tunaamini tume itahakikisha inashirikiana katika kutenda haki hiyo ili wagombea watakaochaguliwa wawe wamepita kwa uhalali na si kufanyiwa kwa utofauti”. SOMA: INEC yafungua milango fomu za udiwani Geita
“Kama kanisa tunaamini uchaguzi huu kwa kuwa tumemshirikisha Mungu kwa maombi, tutawapata viongozi watakaoteuliwa na Mungu kuwaongoza Watanzania kuleta mabadiliko ya maendeleo kama ya kielimu, afya, kilimo na barabara,” alieleza.
Mchungaji Zitto pia amewaomba viongozi wa dini kuwahimiza waumini wao kumtanguliza Mungu kwenye maombi katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi ili uweze kuwa wa haki na uwazi kwa vyama vyote vya siasa vilivyojitokeza na tuwapate walio sahihi kwa ajili ya taifa.
Alisema maombi hayo ni pamoja na kuiombea amani huku akiwataka waumini waliojiandikisha kuhakikisha wanatumia haki yao ya kimsingi kwenda kupiga kura. Pia, aliwataka wananchi kuepuka vishawishi vya rushwa vinavyoweza kuchangia kuwapata viongozi wasio sahihi.



