INEC yavionya vyama sheria za uchaguzi

KIGOMA; TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetaka viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kufuata sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi zilizowekwa, ili kuwasilisha malalamiko yao badala ya kufanya vurugu ambazo zitasababisha kuvuruga uchaguzi.

Mwenyekiti INEC, Jaji  Jacobs Mwambegele amesema hayo katika mkutano wa wadau wa uchaguzi wa Mkoa Kigoma na tume hiyo kuelekea uzinduzi wa uboreshaji daftari la wapiga kura utakaofanyika mkoani Kigoma Julai Mosi mwaka huu, ambapo Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi..

Jaji Mwambegele amesema kuwa tume imejipanga kuhakikisha inashughulikia malalamiko yote ambayo yatapokelewa kutoka kwa wadau wa uchaguzi na  kwa kuanza uboreshaji wa daftari la wapiga kura, amewataka wadau wote wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuboresha taarifa zao.

Advertisement

Isome pia:https://habarileo.co.tz/nida-si-lazima-uboreshaji-daftari-wapigakura/

Kwa upande wake Mkurugenzi wa INEC, Ramadhani Kailima amesema taratibu kwa ajili ya uzinduzi wa  uboreshaji wa daftari la wapiga kura yamekamilika, huku akiwataka wananchi na wadau wote kujitokeza kuboresha taarifa zao, ili waweze kushiriki uchaguzi mkuu.

Kailima amewaonya viongozi wa vyama vya siasa, wananchi, waandishi wa habari na wadau wengine wa uchaguzi kuacha kutoa maneno ya upotoshaji kuhusu uhalali wa wajumbe wa tume, sheria na taratibu za uchaguzi kwani kila kitu kinatekelezwa kwa mujibu wa sheria za nchi na sheria za uchaguzi zilizopo.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/inec-haina-mamlaka-usimamizi-uchaguzi-mitaa/

Wakitoa maoni yao kwenye mkutano huo wadau wa uchaguzi akiwemo Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya kiserikali ya Green Shadow, Ignus Kilongola ameitaka Tume Huru ya Uchaguzi kutenga bajeti kwa ajili ya asasi za kiraia kutoa elimu ya uchaguzi na uhamasishaji jamii masuala ya uchaguzi, badala ya suala hilo kuachiwa asasi zitafute fedha zenyewe.

Kwa upande Katibu wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa Kigoma, Yunus Luhonvya amesema kuwa ni muhimu INEC kuangalia kipengele cha kulipa mawakala, wakati wa uboreshaji daftari na wakati wa upigaji kura, kwani vyama vingi vya siasa havina uwezo wa kugharamia mawakala kutoka kwenye vyama vyao.

/* */