Jifunzeni kwa Tunduma matumizi ya mapato ya ndani-Ummy
SONGWE, Tunduma, Waziri wa afya Ummy Mwalimu amezitaka Halmashauri nchini kuiga mfano mzuri wa Halmashauri ya mji Tunduma kutumia mapato ya ndani kuajiri Watumishi wa afya wa mkataba Ili kupunguza changamoto ya vifo vya mama na mtoto vinavyotokana na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa Watalaamu wa afya.
Waziri Ummy alisema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa wa afya pamoja na viongozi wa Halmashauri ya mji Tunduma katika kituo Cha afya Cha Tunduma kilichopo Wilaya ya Momba, wakati akiendelea na ziara yake ya siku Tatu katika Mkoa wa Songwe.
“Nimpongeze Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Tunduma pamoja na Mkurugenzi Mtendaji kwa kutumia vizuri mapato ya ndani kuajiri Watumishi wa afya wa mkataba 52 ambao wameongeza nguvu na kupunguza changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga ”
Hili ni jambo zuri sana Halmashauri nyingine nchini ziige Ili kutatua changamoto za upungufu wa Watalaamu wa afya ambazo hupelekea Wananchi wetu hasa akina mama na watoto kukosa huduma” amesema Waziri Ummy.
Amesema fedha za mapato ya ndani wanazozikusanya zinatoka kwa Wananchi, Hivyo kuzitaka Halmashauri Nchini kuzitumia kutatua kero mbalimbali za Wananchi hasa kwenye kada ya Afya wakati Serikali ikiendelea kuajili kidogo kidogo.
” haina maana unakusanya mapato mengi alafu unashindwa kutatua kero za Wananchi, Mkurugenzi wa Halmashauri na Mwenyekiti Naomba mwendelee kufanya Hivyo,
waambieni pia wadau wenu wa maendeleo kuhusu changamoto zilizopo kwenye afya Ili wasaidie kuajiri Watumishi wa afya wa mkataba, wasitumie fedha kwenye semina, matangazo na makongamanono pekee” amesema Waziri Ummy.