JKCI kuimarisha matibabu ya moyo Burkina Faso

DAR ES SALAAM; TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Burkina Faso wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika kutoa huduma bobezi ya matibabu ya magonjwa ya moyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam,  Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dk Peter Kisenge, mara baada ya kusaini makubaliano hayo amesema makubaliano yataimarisha utoaji wa huduma za matibabu ya moyo nchini Burkina Faso na kuokoa maisha ya wananchi wenye matatizo ya moyo.

“Tumekubaliana kusaidia katika kufanya tatifi, kuwafundisha wataalamu wa afya wakiwemo madaktari, wauguzi na wataalamu wa vifaa tiba jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo na namna ya kutumia vifaa tiba vya moyo pia watawatuma wagonjwa ambao wameshindwa kuwafanyia upasuaji waje kutibiwa katika taasisi yetu,” amesema.

Amesema katika kutoa mafunzo ya kuwatibu wagonjwa ya moyo kuna wataalamu ambao wataenda Burkina Faso kufundisha na kuna wataalamu kutoka nchini humo watakaokuja kujifunza JKCI.

Dk Kisenge amesema kuhusiana na upatikanaji wa vifaa tiba wamekubaliana wanunue katika Bohari ya Dawa (MSD) ambao ni wasambazaji wa vifaa hivyo katika taasisi hiyo.

“Kwa namna ya kipekee namshukuru sana Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha tiba ya magonjwa ya moyo katika taasisi yetu kitu ambacho kimesababisha nchi mbalimbali kuja kujifunza namna ya kutoa matibabu ya moyo katika nchi zao pia kuwaleta wagonjwa wao kutibiwa JKCI.

“Pia ninamshukuru Rais wa Bukina Faso ,Kapteni Ibrahimu Traore kwa kuiamini nchi yetu na kuwatuma wataalamu wake ambao tumesaini makubaliano nao ili nao kupitia sisi wawe taasisi bora ya matibabu ya moyo na kufika hatua tuliyoifikia sisi na leo tumeingia katika historia na Burkina Faso ya kutangaza utalii tiba ambao umekuja katika afya”, amesema Dk Kisenge.

Kwa upande wake Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore ambaye kwa mara ya pili ameongoza timu hiyo ya wataalamu kuja hapa nchini alisema siku ya kwanza walipotembelea JKCI walivutiwa kwa huduma wanazozitoa pamoja na uhusiano mzuri wa uongozi wa manejimenti uliokuwepo baada ya kurudi nchini kwao walivichukuwa hivyo vyote na kuvifanyia kazi.

“Ninawashukuru maraisi wetu wa Burkina Faso,Kapteni Ibrahimu Traore na wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuwa tayari kuimarisha huduma za afya katika nchi zao, nimevutiwa na JKCI kwani haitoi huduma tu Tanzania bali Afrika nzima ndiyo maana nasi tumekuja kujifunza. Tunawategemea sana katika mafunzo, tafiti na matibabu ya moyo kwa afya za watu wa Burkina Faso”, amesema Traore.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button