Johari aeleza sheria za uchaguzi zilivyorekebishwa

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari ameshangazwa na madai ya watu kudai mabadiliko kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika wakati serikali imeshafanya marekebisho ya sheria mbili kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Alisema haoni sababu ya watu kudai uboreshaji wa sheria za uchaguzi mkuu kwani serikali imeshafanya uboreshaji wa sheria.

Johari alisema hayo jana katika Kongamano la Kitaifa la Sheria lilioandaliwa na Chama cha Mawakili wa Serikali lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza katika kongamano hilo Johari alisema mabadiliko ya Sheria za Uchaguzi katika mwaka 2024 yalifanyika kutokana na maombi ya wadau vikiwemo vyama vya siasa na walishirikishwa kutoa maoni kuhusu sheria hizo.

Alisema baada ya maombi hayo, serikali ilikusanya maoni kuhusu na kufanya marekebisho katika sheria kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Alisema lilitunga sheria mbili ambazo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais Wabunge na Madiwani ya 2024 na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na ni wito uliotoka kwa vyama vya siasa na wadau wengine.

Alisema kupitia kikosi kazi kilichoongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala cha kukusanya maoni kuhusu demokrasia na vyama vingi nchini walipendekeza kutungwa kwa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi.

“Vyama vya siasa vyote vilishiriki katika mchakato mzima wa mabadiliko ya sheria za uchaguzi zikiwemo sheria ya vyama vya siasa hivyo nashangaa kuona wanaosema hakuna reform (mabadiliko) zilizofanyika kuhusu masuala ya uchaguzi na tume huru ya uchaguzi,” alisema Johari.

Alisisitiza: “Serikali hii ni sikivu na imefanya maboresho mengi baada ya tume ile ya Profesa Mukandala.”

Johari alisema vyama pia vilitoa mapendekezo ya kuunganisha sheria ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani na uchaguzi wa serikali za mitaa na kuiborehsa sheria ya vyama vya siasa kwa kuimarisha makundi maalumu.

Aidha, alimshukuru Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika tukio hilo muhimu la kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu sheria za uchaguzi.

Pia, aliwataka wananchi kutumia fursa ya kongamano hilo kujifunza na kujiandaa na maboresho hayo yaliyofanyika katika sheria hasa wakati huu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Alisema kongamano hilo ni la kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwa Chama cha Mawakili wa Serikali na lengo kuu ni kuwajengea uelewa wananchi kuhusu sheria zilizofanyiwa maboresho kuelekea uchaguzi.

Rais wa Chama Cha Mawakili wa Serikali (PBA), Bavoo Yunusu alisema kongamano hilo linalenga kujenga uelewa mpana kwa wananchi kuhusu masuala ya sheria kuelekea uchaguzi mkuu ili washiriki kikamilifu kwenye uchaguzi

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button