NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio amesema moja ya malengo ya Kongamano la Kimataifa la Jotoardhi (ARGeo-C10) linalofanyika Tanzania ni kuwezesha Afrika kuongeza kasi ya uendelezaji wa rasilimali ya jotoardhi.
Amesema rasilimali ya jotoardhi ikiendelezwa ipasavyo barani Afrika itatumika kwa namna mbalimbali ikiwemo kuzalisha umeme pamoja na matumizi mengine ya moja kwa moja kwenye Sekta ya Kilimo na Ufugaji.
Dk. Mataragio amesema hayo jijini Dar es Salaam katika hafla ya ufungaji wa mafunzo ya Jotoardhi kwa washiriki wa Kongamano la Kimataifa la ARGeo-C10 linaloendelea jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya programu za kongamano hilo.
“Tanzania ina maeneo mengi yaliyotambuliwa yenye viashiria vya Jotoardhi na tayari Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TGDC) inaendelea na shughuli za utafiti katika maeneo mbalimbali ikiwemo Songwe, Kiejo-Mbaka na Ngozi,” amesema Dk. Mataragio.
Ameeleza kuwa, kwa Tanzania kuweka mkazo kwenye uzalishaji wa umeme kwa kutumia chanzo cha Jotoardhi kunaendana na malengo ya dunia ya kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa hewa ya ukaa kwani Jotoardhi ni nishati safi.
Ametaja mafunzo yaliyotolewa katika Kongamano la Kimataifa la ARGeo-C10 kuwa ni pamoja na uendelezaji wa mashapo ya Jotoardhi na teknolojia mpya, matumizi ya moja kwa moja ya jotoardhi katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na ufugaji hasa wa samaki pamoja na athari za masoko ya kaboni (carbon markets).
“Kwa kupitia mafunzo haya tumezidi kujenga uwezo kwa vijana wa kitanzania ili kuweza kuendeleza rasilimali ya Jotoardhi tuliyonayo kupitia Wataalam wabobezi katika masuala yanayohusu nishati hii,” amesema Mataragio.
Ametaja nchi mbalimbali zilizoshiriki mafunzo hayo zinazojihusisha na rasilimali ya jotoardhi kuwa ni Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia, Nigeria, Cameroon na New Zealand ambapo Tanzania imeweza kupata uzoefu kutoka nchi nyingine ziliopiga hatua kubwa katika uendelezaji wa nishati hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wa mafunzo hayo, Agnelli Kafuwe kutoka nchini Zambia, amesema kuwa yatasaidia katika kuisimamia sekta ya Jotoardhi kwani wameongeza uelewa kuhusu nishati hiyo ikiwemo fursa na changamoto zinazoweza kutokea katika usimamizi wake.
Amesema kuwa nishati ya Jotoardhi haihusishi umeme peke yake hivyo lazima matumizi yake ya moja kwa moja yanayoweza kuboresha maisha ya watu yapewe kipaumbele ikiwemo kupitia katika Sekta ya Kilimo.
Ametoa wito kwa nchi za Afrika kuunganisha nguvu ili kuweza kupiga hatua zaidi katika uendelezaji wa Nishati ya Jotoardhi kama ilivyo falsasa ya ujamaa ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
Comments are closed.