Kabila amkosoa Rais Tshisekedi

DRC: RAIS wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Joseph Kabila amesema kuwa uongozi mbaya wa mrithi wake, Rais Felix Tshisekedi umechangia kuzidisha mzozo unaoendelea mashariki mwa nchi hiyo.

Kabila alieleza kuwa mgogoro huo umechangiwa zaidi na hatua za serikali ya Tshisekedi ambazo zimeimarisha hali ya ukosefu wa usalama katika eneo hilo.

Katika makala ya maoni aliyoiandika katika gazeti la Afrika Kusini la Sunday Times, Kabila amesema kuwa mzozo wa mashariki ya DRC haujazoeleka tu kwa sababu ya kundi la waasi la M23, linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, bali pia kutokana na mvutano mkubwa kati ya Kinshasa na Kigali.

Hali hii imeongeza ghasia na kupelekea hali ya kisiasa kuwa tete zaidi.

Wapiganaji wa M23 wamekuwa wakiteka maeneo kadhaa ya mashariki mwa DRC kwa haraka katika wiki zilizopita, na hadi sasa wanadhibiti maeneo makubwa yenye utajiri wa rasilimali.

Hali hiyo imezua hofu kubwa kwamba mzozo huo unaweza kusambaa zaidi na kuvuka mipaka ya DRC, na kuathiri nchi nyingine za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Kabila aliongeza kuwa tangu Tshisekedi aingie madarakani mwaka 2019, baada ya kushinda uchaguzi wa 2018, hali ya kisiasa nchini DRC imeendelea kuzorota na kufikia hatua ya mpasuko mkubwa.

Rais huyo wa zamani alieleza kuwa hali hiyo inaonekana kuwa mbaya zaidi kutokana na vitendo vya serikali ya Tshisekedi.

Aidha, Kabila alishutumu uchaguzi wa Desemba 2023 ambao ulimpa Tshisekedi muhula wa pili, akisema kuwa uchaguzi huo ulikuwa na “udanganyifu.”

Alisisitiza kuwa utawala wa Tshisekedi umekandamiza upinzani wa kisiasa, na kumtaja Rais Tshisekedi kama “dikteta.” Kabila alieleza kuwa vitisho, kukamatwa kwa watu kinyume cha sheria, mauaji ya kiholela na kufukuzwa kwa wanasiasa, waandishi wa habari, na viongozi wa mashirika ya kiraia, ikiwa ni pamoja na viongozi wa makanisa, ni miongoni mwa sifa za utawala wa Tshisekedi.

CHANZO: VOA

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button