Kabila aondolewa kinga ya kushtakiwa DRC

DRC: BARAZA la Seneti nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) limemvua rasmi kinga ya kutoshitakiwa Rais wa zamani Joseph Kabila, hatua inayomruhusu kushitakiwa kwa tuhuma za kusaidia waasi wa kundi la M23 wanaodhibiti baadhi ya maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo.

Katika kikao kilichofanyika jana mjini Kinshasa, jumla ya kura 88 ziliidhinisha kuondolewa kwa kinga hiyo, hatua inayotajwa kuwa ya kihistoria katika siasa za taifa hilo.

Spika wa Seneti, Jean-Michel Sama Lukonde, alitangaza matokeo ya kura hiyo na kusema kuwa sasa hakuna tena kizuizi cha kisheria kwa Kabila kufikishwa mahakamani.

“Baraza la Seneti limeamua kwa wingi wa kura kuruhusu Joseph Kabila kufikishwa mahakamani na kuondolewa kinga yake ya kutoshtakiwa,” alisema Lukonde.

Tuhuma dhidi ya Kabila zinatolewa na serikali ya sasa chini ya Rais Félix Tshisekedi, ikidai kuwa Kabila aliwahi kushirikiana kwa njia mbalimbali na kundi la waasi la M23, ambao wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara mashariki mwa DRC.

Waasi hao, wanaoshutumiwa kupokea msaada kutoka nje ya nchi, wamekuwa wakifanya mashambulizi dhidi ya raia na majeshi ya serikali kwa kipindi kirefu, hali iliyochangia kuendelea kwa machafuko na ukosefu wa amani katika eneo hilo la taifa hilo kubwa barani Afrika.

Hatua ya Seneti kuondoa kinga ya Kabila inachukuliwa na wachambuzi wa masuala ya siasa kama ukurasa mpya wa uwajibikaji, huku wengine wakiona kama ni mkakati wa serikali ya sasa kujitofautisha na tawala zilizopita na kuimarisha uadilifu serikalini.

SOMA: Waasi M23 waanza safari ya Butembo

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button