Kagera wapewa muongozo miche bora ya kahawa

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila, ametoa wito kwa halmashauri zote mkoani Kagera, kuhakikisha zinatenga asilimia 20 itokanayo na kodi ya kahawa kuzalisha miche bora ya kahawa.
Ametoa wito huo wakati akifungua semina ya mafunzo kwa viongozi vya vyama vya msingi (Amcos), yaliyoandaliwa na Tume ya Ushindani (FCC).
Mafunzo hayo yamelenga kujenga uelewa kwa viongozi wa vyama vya msingi na viongozi wa ushirika, juu ya majukumu ya Tume ya Ushindani katika kulinda mazao yao na kuwaongezea uchumi.
Alisema msimu huu wa Kahawa 2021/2022, tayari halmashauri za Mkoa wa Kagera zimepokea mapato yatokanayo na kahawa, lakini atashangaa kuona hakuna shukurani inayorudi kwa wakulima, wakati wao ni sehemu ya mapato hayo.
Alisema kuna utamaduni ambao umejengeka kuwa mbegu kutoka nje ya nchi ndizo bora, wakati ndani ya halmashauri na tasisi Kuna wataalamu ambao wanaweza kuzalisha mbegu bora, zinazoweza kumsaidia mkulima, kupata mavuno Bora.
” Wakurugenzi naomba mhakikishe asilimia 20 ya mapato ya kahawa inarudi kwa wakulima wenu, kwa sababu wao ni sehemu ya kipato hicho, nisingependa kuona halmashauri haina vitalu vya miche ya kahawa na miche hiyo wakulima waipate bure, “alisema Chalamila.
Alivitaka viwanda vinavyokoboa na kusaga kahawa ya unga, kuongeza ubunifu katika bidhaa ya kahawa iliyokobolewa, ili kupata masoko zaidi, kwani amegundua kuwa viwanda vingi vinavyouza kahawa iliyoongezewa thamani vinaendana na mtindo wa zamani na hakuna ubunifu wowote.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa FCC, Magdalena Utto, alisema kahawa ni biashara kubwa ulimwenguni, hivyo kazi ya tume ni kuhakikisha kahawa ya Tanzania inayafikia masoko bora na kumnufaisha mkulima.