WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) hiyo kuhakikisha miradi ya ujirani mwema inayotekeleza ijikite katika kutatua changamoto ya wanyama wakali na waharibifu.
Kairuki amesema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka hiyo yaliyopo Mkoani Morogoro ambayo ililenga kusikiliza changamoto na kutoa utatuzi ili kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka.
Kairuki ametaja hatua hizo ni pamoja na kujenga vizimba na kutoa vitendea kazi kama pikipiki ili viweza kupunguza changamoto hiyo.
Amesema TAWA ifanye minada ya vitalu vya uwindaji kwa wakati na kwa kufuata kalenda na pia kujifunza kutokana na matokeo ya minada iliyopita kwa kutatua changamoto zilizojitokeza na kuboresha hadhi za vitalu wanavyovinadi ili kuongeza mapato ya Serikali.
Waziri Kairuki pia ameipongeza Mamlaka hiyo kwa usimamizi mzuri wa rasilimali za wanyamapori.
“Nawapongeza TAWA kwa usimamizi mzuri wa rasilimali ya wanyamapori kwa kuzingatia kuwa ni taasisi ambayo haina muda mrefu tangu kuanzishwa kwake,” amesema Kairuki.
Soma hapa: http://TAWA kuimarisha ulinzi wa wananchi dhidi ya wanyamapori
Waziri huyo pia ametaka uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Miongozo na taratibu kwa watumishi katika kutimiza majukumu yao ili kuboresha utendaji kazi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka hiyo, Mabula Misungwi Nyanda licha ya kumkaribisha alimshukuru Waziri kwa kutenga muda wake na kuitembelea Mamlaka hiyo na ameahidi utekelezaji wa maelekezo yote aliyoyatoa.
Awali, Kaimu Naibu Kamishna anayeshughulikia huduma za uhifadhi, Mlage Kabange ametoa taarifa kuhusu maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka hiyo akibainisha mafanikio pamoja na jitihada zinazofanywa katika kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu.
Katika ziara hiyo, Waziri Kairuki aliambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Fortunata Msoffe, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Wizara ya Maliasili na Utalii, Abdallah Mvungi pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Wizara ya Maliasili na Utalii, Lucy Saleko.