TUNISIA : RAIS wa Tunisia, Kais Saied, amemfuta kazi Waziri Mkuu Kamel Madouri wakati taifa hilo likikumbwa na matatizo makubwa ya kiuchumi.
Madouri, aliyeteuliwa mwezi Agosti mwaka jana, ameondolewa katika nafasi hiyo wakati Tunisia inakabiliwa na changamoto za kiuchumi.
Nafasi ya Madouri imechukuliwa na Sarra Zaafrani Zenzri, ambaye ni mwanasiasa aliyewahi kushika wadhifa wa Waziri wa Ujenzi. SOMA: Mgombea urais atupwa jela Tunisia
Zaafrani, mwenye umri wa miaka 62, anakuwa mwanamke wa pili kushika wadhifa wa Waziri Mkuu wa Tunisia baada ya Najla Bouden, ambaye alishikilia nafasi hiyo kati ya Oktoba 2021 hadi Agosti 2023.
Hata hivyo, Umoja wa Mataifa na asasi za kiraia zinaendelea kuilaumu serikali ya Tunisia kwa kukandamiza demokrasia na kupuuzia haki za binadamu, hali inayozidi kuzua wasiwasi ndani ya taifa hilo.
Kwa sasa, Tunisia inakadiriwa kuwa na raia wasiopungua milioni 12, na inakutana na changamoto za kiuchumi kama vile upungufu wa bidhaa muhimu kama sukari na unga wa ngano, huku ukosefu wa ajira ukiwa bado ni changamoto kubwa.