Kamati yaridhia kuanzishwa kwa mji mdogo wa Misigiri

KAMATI ya Ushauri ya Wilaya ya Iramba, ikiongozwa na mwenyekiti ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Suleiman Mwenda imepitisha kwa kauli moja mapendekezo ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Misigiri.
Uamuzi huo ulifanyika katika kikao chake cha kupitia rasimu na mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika Jumatano Machi 5, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri.
“Halmashauri iandae mpango mji mzuri utakao wezesha mji kuwa Katika mpangilio mzuri na kukaa kibiashara,” amesema DC Mwenda.

Katika kikao hicho, wajumbe walipendekeza kuundwa kwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Misigiri kwa lengo la kuharakisha maendeleo na kuimarisha ukuaji wa mji huo.
“Mwenyekiti, wewe ni shahidi kuwa wilaya yetu ilianzishwa kabla ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1958. Hata hivyo, tangu tupate uhuru, Kiomboi haijakua kwa kasi kutokana na umbali wake kutoka barabara kuu. Kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Misigiri kutachochea maendeleo kwa haraka,” alisisitiza Geofrey Tungu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi, aliwapongeza wajumbe kwa mawazo yao yenye lengo la kuikuza na kuendeleza wilaya hiyo.
“Nakupongeza DC Mwenda kwa kuendesha kikao chenye hoja zenye tija kwa maendeleo ya Wilaya yetu. Jambo hili ni la manufaa kwa wananchi, na siku za baadaye, jamii itakushukuru kwa mchango wako wa kimaendeleo,” alisema Msengi.
Aidha, Kamati ya Ushauri ya Wilaya pia imeridhia mapendekezo ya kuanzishwa kwa kata mpya nane (8), kutoka kata za awali 20. Kata zilizopendekezwa ni Kisharita, Ushora, Ujungu, Kisana, Wembere, Nsunsu, Mseko, na Tyeme.
Hatua Hii Itachochea Maendeleo ya Iramba
Kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Misigiri kunatarajiwa kuvutia wawekezaji, kuboresha huduma za kijamii, na kuimarisha miundombinu katika wilaya hiyo, hivyo kuifanya Iramba kuwa na maendeleo endelevu.



