KAMATI ya Huduma za Kijamii kutoka Shehia ya Kizimkazi Dimbani Zanzibar, imetembelea Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani ili kujifunza na kujionea miradi ya miundombinu iliyotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ( TASAF).
Akizungumzia kuhusu ziara hiyo Mratibu kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Makame Ally Haji amesema hayo wakati wa ziara hiyo yenye ujumbe wa watu 20 kutoka Zanzibar.
Amesema kwa kuiona miradi miwili iliyotekelezwa na Tasaf ya Soko Kuu la Utete na Mradi wa madarasa manne, matundu nane ya vyoo na ujenzi wa bweni kwenye shule ya sekondari ya wasichana ya Dk Samia Suluhu Hassan, wameweza kupata mambo mengi mapya kuhusu utekelezaji wa mradi huo na wao kutoa uzoefu wao.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa soko Kuu la Utete kwa Kamati ya Usimamizi wa Jamii kwa miradi ya ujenzi Zanzibar, Mtendaji wa Kata ya Utete, Edmund Marcell amesema halmashauri hiyo ilipokea zaidi ya Sh milioni 125 toka Tasaf kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo ulioanza februari tisa mwaka jana.
” Fedha hizo ziliwezesha ujenzi wa soko mpaka kufikia hatua ya kuezeka. Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kutokana na mapato yake ya ndani iliongeza sh milioni 46 zilizotumika kwenye hatua ya umalizaji wa soko pamoja na ujenzi wa choo,” amesema.
Pia amesema wananchi wa Kata ya Utete walishiriki kufanya shughuli mbalimbali wakati wa ujenzi wa soko zilizokadiriwa kuwa na kiasi cha sh milioni 2.7 hivyo kufanya jumla ya gharama za mradi kuwa zaidi ya Sh milioni 174.
Kwa upande wake Mratibu wa Tasaf wilaya hiyo, Pamella Birukila alisema halmashauri ya wilaya ya Rufiji imeendelea na utekelezaji wa miradi ya miundombinu inayotekelezeka katika kata ya Mgomba na Utete.
” Miradi hii imetekelezwa ikiwa ni hitaji la jamii baada ya miundombinu iliyopo kuwa imechakaa sana au kutokuwepo kabisa.
” Jumla ya zaidi ya sh milioni 361 zimepokelewa na halmashauri ya Wilaya ya Rifiji zikiwa ni kwa ajili ya miradi ya miundo mbinu,” amesema
Amesema changamoto zilizojitokeza ni pamoja na kupanda kwa bei ya vifaa kama nondo na saruji pamoja na walengwa kutokuwa na namba za NIDA ili kuwawezesha kuunganishwa na malipo kwa njia ya kielectroniki.