Kamera kunasa wanaotanua, kuzungumza na simu barabarani

DAR ES SALAAM; MUAROBAINI wa madereva wanaosababisha msongamano na foleni kwa kutanua na kuzungumza na simu katika barabara mbalimbali kwenye wilaya mbili za Ubungo na Kinondoni mkoani Dar es Salaam umewadia kwa kamera 60 kufungwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule akishirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando wamefanikisha kupata kamera 60 za kisasa zinazohamishika zitakazofungwa katika barabara za Bagamoyo na Mwai Kibaki ili kudhibiti madereva wasiofuata sheria za barabarani.

Mtambule alisema wilaya hizo mbili mkoani humo wamebaini chanzo cha msongamano ni uzembe wa madereva kutokuwa na nidhamu na kutofuata utaratibu wa sheria za barabarani ikiwemo kutanua na kuzungumza na simu muda mrefu wawapo barabarani.

“Barabara ya mistari miwili madereva wanatanua hadi mistari mitano, hii inafanya foleni iwe kubwa na kuleta msongamano, wengine wanazungumza na simu muda mrefu, sasa tumeleta dawa tunafunga kamera na tutawakamata wote na kuwafunga, kulipa faini au kufutiwa leseni,” alisema Mtambule.

Alisema katika kamera hizo 60, zitafungwa 20 katika Barabara ya Mwai Kibaki na kuwa kipande chote cha barabara hiyo kamera hizo zitawamulika madereva wote wazembe, hivyo kurahisisha kuwakamata.

Kamera nyingine 30 zitafungwa Barabara ya Bagamoyo ili kudhibiti uzembe wa madereva hao wanaosababisha foleni na msongamano unaoweza kuepukwa na kuwa katika kila kamera itafungwa umbali wa meta 500 kati ya moja hadi nyingine.

“Yeyote anayezungumza na simu wakati akiendesha, tunakwenda kumshika, tunafunga kamera umbali wa meta 500 kati ya moja hadi nyingine na kila dereva mzembe na anayetanua katika barabara tutamkamata na kuwapeleka mahakamani,” alisema Mtambule.

Alitoa mwito kwa madereva wote ama wa magari ya serikali au binafsi watambue hilo vinginevyo, watakaoendelea kukiuka sheria na taratibu, watalipa faini, kufungiwa leseni za udereva au kufungwa jela.

Wiki iliyopita, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Msando alisema katika wilaya hiyo watafunga kamera katika Barabara ya Makongo kwenda Goba kupitia Survey ili kuwabaini madereva wasiotii sheria ambao wanaosababisha kero kwa watumiaji wake kutokana na msongamano mkubwa.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button