Kamil Idris ateuliwa Waziri Mkuu mpya Sudan

KHARTOUM : MKUU wa Jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, amemteua afisa wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kamil Idris, kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo.
Idris ambaye ni mwanadiplomasia na msomi aliyewahi kuwania urais, amewahi pia kushikilia nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Haki Miliki (WIPO), pamoja na kuhudumu katika ubalozi wa kudumu wa Sudan kwenye Umoja wa Mataifa.
Uteuzi wake unakuja kuchukua nafasi ya mwanadiplomasia mkongwe Dafallah al-Haj Ali, ambaye aliteuliwa na Burhan mwishoni mwa Aprili mwaka huu na kuhudumu kwa muda wa chini ya wiki tatu kama kaimu Waziri Mkuu.
Kuteuliwa kwa Idris kunakuja wakati Sudan ikiendelea kukumbwa na hali tete ya kisiasa na kiusalama tangu mapinduzi ya kijeshi na kuendelea kwa machafuko kati ya jeshi na makundi yenye silaha.