Kampeni Mtu ni Afya yapamba moto Iringa

KAMPENI ya ‘Mtu ni Afya’ imeanza kwa kasi mkoani Iringa ikihusisha uhamasishaji wa wakazi wa mkoa huo kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, ameongoza jitihada hizi, akisisitiza umuhimu wa mazoezi ya pamoja kama njia ya kudhibiti ongezeko la magonjwa haya.

Kampeni hiyo,inayofanyika katika kata mbalimbali za halmashauri tano za mkoa huo, inabeba kauli mbiu ya “Fanya Kweli, Usibaki Nyuma” na inaongozwa na Balozi wa kampeni hiyo, msanii maarufu Mrisho Mpoto.

SOMA: Serikali yazungumzia udhibiti magonjwa ambukizi

“Katika kutekeleza awamu hii ya pili ya kampeni, tumeweka utaratibu wa kufanya mazoezi ya pamoja mara mbili kila mwezi katika halmashauri zote kama sehemu ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu,” alisema Serukamba.

Serukamba aliongeza kuwa kampeni hiyo itajikita pia katika kuhakikisha usafi wa mazingira, hasa kwa kutoa elimu juu ya hedhi salama kwa watoto wa kike na huduma za usafi shuleni. Hii inalenga kusaidia jamii kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

Mrisho Mpoto, maarufu kwa jina la ‘Mjomba’ alitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kuhusu kampeni hiyo na kusema: “Tumekuja Iringa tukitambua kwamba mkoa huu ni mshindi wa kampeni ya usafi wa mazingira kitaifa, tuzo iliyotolewa wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya kampeni ya Mtu ni Afya, Mei 9, huko Kibaha, Pwani.”

SOMA: Serikali kupunguza uhaba watumishi wa afya

Mpoto alieleza kuwa wako Iringa ili kuongeza hamasa kwa wakazi wa mkoa huo kushiriki kwa nguvu katika kampeni hiyo. Mkuu wa Mkoa wa Iringa alisema kuwa wana uhakika mkoa huo utashinda tena katika kampeni ya kitaifa.

Wakiwa mkoani humo, Mpoto alisema kuwa mbali na kuhamasisha jamii kufanya mazoezi, kampeni hiyo pia inajikita katika kuhamasisha matumizi ya vyoo bora katika kaya na shule za msingi na sekondari. Pia itasisitiza umuhimu wa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.

“Kampeni ya Mtu ni Afya inajikita pia katika suala la vyoo bora kama sehemu muhimu ya kuimarisha afya ya jamii. Usafi wa mazingira, hususan matumizi ya vyoo bora, ni msingi wa kuzuia magonjwa ya kuambukiza kama vile kipindupindu, kuhara, na magonjwa mengine yanayohusiana na uchafu,” alisema Mpoto.

 

View this post on Instagram

 

A post shared by HABARILEO (@habarileo_tz)

Habari Zifananazo

Back to top button