“Kanuni zilifuatwa kuengua wagombea”

MSIMAMIZI wa uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini, Kisena Mabuba amesema sheria na taratibu za uchaguzi ndizo zilizosababisha wagombea wa nafasi ya mwenyekiti na wajumbe wa serikali za mitaa kukosa sifa na kuenguliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma, msimamizi huyo wa uchaguzi amesema mchujo huo wa wagombea wenye sifa umehusisha vyama 17 vilivyosimamisha wagombea kwenye uchaguzi huo ikiwemo CCM ambayo wajumbe wake pia wameenguliwa kwa kukosa sifa.

Advertisement

Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kigoma Mjini Kisena Mabuba (katikati) akiwa na wasaidizi wake katika kikao ma waandishi wa habari kutoa ufafanuzi zoezi la uteuzi wa wagombea wa serikali za mitaa

Bila kutaja idadi kwa vyama vyote amesema kuwa Chama cha ACT Wazalendo ambacho kilisimamisha wagombea wa nafasi ya mwenyekiti na wajumbe kwa mitaa yote 68 ya jimbo la Kigoma Mjini wagombea wake tisa wameenguliwa kwa kukosa sifa.

Msimamizi huyo wa uchaguzi amesema kuwa miongoni mwa vigezo vilivyowafanya wagombea hao kukosa sifa ni Pamoja na kushindwa kukamilisha maelekezo ya kujaza fomu za uteuzi na wengine kukosa sifa kwa sababu ya masuala ya utata wa uraia wao.

Frank Ruhasha (kushoto) msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kigoma Mjini Chama cha ACT Wazalendo akizungumza na waandishi wa habari

Akizungumzia kadhia ya kuenguliwa kwa wagombea wa chama chao msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini wa Chama cha ACT Wazalendo, Frank Luhasha amesema kuwa walisimamisha wagombea zaidi ya 400 kwa nafasi zote zilizotangazwa kwenye mitaa yote 68 ya jimbo la Kigoma Mjini lakini walioteuliwa ni wagombea 70 pekee.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Kigoma Mjini, Omari Gindi amesema kuwa katika chama chao nafasi ya mwenyekiti wameenguliwa wagombea wanne na wajumbe 12 na kwamba sababu walizoambiwa za kukosa sifa kwa wajumbe hao siyo ya kikanuni yanayoweza kumuengua mgombea hivyo Chadema taifa wametoa maelekezo kwamba watatoa tamko kuhusu jambo hilo.

Omari Gindi, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Kigoma Mjini