Katavi wapanga kujenga uwanja wa mpira

HALMASHAURI ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, katika kuongeza vyanzo vya mapato inakusudia bajeti ijayo kutenga fedha kwa ajili ya kujenga uwanja wa mpira, ili iweze kujiingizia mapato.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Shaban Juma, wakati akijibu hoja ya Diwani wa Kata ya Tongwe, Frank Kibigasi katika kikao cha kawaida cha Baraza la madiwani aliyetaka kujua mikakati ya Halmashauri kubuni chanzo cha mapato kupitia michezo na kusema kuwa tayari ameshampatia maelekezo Ofisa Utamaduni kutafuta eneo kubwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa kisasa.

“Katika dunia ya leo sehemu nyingi masuala ya michezo wanayapa umuhimu, ila sisi wilayani hapa hatuna kiwanja cha michezo, tunaangalia eneo zuri ambalo linaweza kuwa kubwa na linafikika na watu kwa ukaribu ili tuweze kuingiza nguvu zetu,” alisema.

Advertisement

 

Diwani Kibigasi ameishauri halmashauri kuanzisha kituo cha kukusanyia ushuru eneo la Ngomalusambo kwa kuwa eneo hilo mazao yanapitishwa kiholela, jambo linaloikosesha halmashauri mapato na kuinufaisha halmashauri nyingine.

Akichangia hoja hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amesema kipaumbele cha Rais Dk Samia Suluhu Hassan ni mapato, hivyo halmashauri inapaswa kujipanga kutokana na mahitaji kuongezeka kila leo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Hamad Mapengo, amemtaka Mkurugenzi kufanyia kazi ushauri uliotolewa na wajumbe wa baraza hilo, ili kuleta ufanisi katika eneo la ukusanyaji mapato.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *